Connect with us

General News

Lady Bee

Published

on

Lady Bee

BERNICE Nduku almaarufu Lady Bee ni miongoni mwa wanasanii wa humu nchini wanaotumia muziki kueneza Ukristo, kuhimiza uadilifu na kupigia chapuo makuzi ya Kiswahili.

Jambo ambalo waimbaji chipukizi wanaweza kujifunza kutokana naye ni kwamba changamoto wanazopitia maishani zinastahili kuwa jukwaa la kuwakomaza na kubadilisha mitazamo yao kuhusu mambo mbalimbali.

Iwapo Lady Bee angesalia kujutia maamuzi ya utotoni yaliyomsukuma kuwa mraibu wa dawa za kulevya, basi angepoteza dira na utajiri wa kipaji chake cha ubunifu kwani asingejulikana hata nje ya mtaa wa Eastleigh (Nairobi) alikozaliwa na kulelewa.

Sasa anavuma kimataifa kutokana na nyimbo zake za Injili na amewahi kupata mialiko ya kuandaa shoo mbalimbali Dubai na nchini Nigeria.

“Tumia hali yako ya sasa kuboresha kesho yako. Usikubali kushindwa na jambo lolote zuri maishani. Jitabirie mambo makuu na usiogope kujaribu,” anasema.

Lady Bee ndiye mwanambee katika familia ya watoto watatu wa Bi Mercy Munee na marehemu Bw Francis Mugo. Alisomea katika shule ya msingi ya St Peter Claver’s jijini Nairobi kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Gathanji, eneo la Nyahururu, Kaunti ya Nyandarua.

Alijitosa katika fani ya muziki mwanzoni mwa miaka ya 1990 akiwa mwanachama wa Jambo Sounds (Jambo Rebels Band). Alijiunga baadaye na kundi la Weavers Band lililomnoa katika upigaji gitaa kabla ya kuelekea Dubai mnamo 2000 kujikuza zaidi kisanaa akiwa na kundi la Bilenge Musica.

Alirejea Kenya katika mwaka wa 2007 na kujiunga na kikundi cha Pro Habo kilichompa jukwaa la kurekodi vibao kadhaa vikiwemo ‘Chali wa Mtaani’, ‘Sema Nami’ na ‘Kumbuka’.

Uimbaji kwa sasa umemfanya kuwa ‘mwalimu’ wa Kiswahili kila anaposhuka ulingoni kutumbuiza mashabiki na waumini makanisani, redioni, runingani, mitandaoni na kumbi nyinginezo.

Tangu aanze safari ya wokovu mnamo 2012, amefyatua zaidi ya nyimbo 30 anazopania kuhifadhi katika albamu nne.

“Niliacha kuimba nyimbo za dunia na kuteua mkondo wa maisha ya wokovu ili kuchochea maono yangu kuwa ndoto zenye thamani. Kufanikisha azma hiyo kulihitaji imani, nidhamu na stahamala,” anaeleza.

Mbali na wimbo ‘Matunda’ alioucharaza kwa ushirikiano na Rebecca Soki na Eunice Njeri, kazi nyingine iliyomkweza juu zaidi kwenye chati ya muziki wa Injili ni kibao ‘John 3:16’.

‘Damu ya Yesu’, ‘Twende Kwa Yesu’, ‘Nakiri’, ‘Hilo Jina’, ‘Ananipenda’, ‘Nakuita Baba’, ‘Yesu Ni Bwana’, ‘Roho Mtakatifu’ na ‘Nakuinua’ ni nyimbo nyinginezo maarufu ambazo Lady Bee amezisana kwa Kiswahili.

Zaidi ya kuwa mwinjilisti, anaendesha pia kampeni maalumu ya kusaidia mayatima na kuwapa vijana ushauri nasaha kupitia mradi ‘Yesu Anaweza Crusade’. Azma yake kuu ni kukuza maadili, kupiga vita ndoa za mapema na dhuluma dhidi ya wanawake, pamoja na kuhamasisha jamii kuhusu masuala ya afya na umuhimu wa kuhifadhi mazingira.

Lady Bee amejaliwa mtoto wa kike, Yvonne Mercy. Anashikilia kuwa siri ya kufaulu katika tasnia ya muziki ni kumtanguliza Mungu katika kila hatua na kumtumikia kwa moyo wote katika hali zote.

“Imani ndiyo hutupa neema na msukumo katika safari ya maisha. Tunampendeza Mungu kupitia imani. Mungu ndiye mwenye nguvu, rehema na mamlaka yote. Mtegemee katika kila jambo,” anashauri.

Comments

comments

Trending