Lamu yafaidi miradi mingi ikikamilishwa
Na KALUME KAZUNGU
MWAKA wa 2021 ulikuwa wa baraka tele kwa kaunti ya Lamu na wakazi kwa jumla kwani ulishuhudia kufunguliwa kwa miradi mikuu ya serikali ya kitaifa iliyotumia mabilioni ya fedha kukamilika.
Miongoni mwa miradi hiyo ni ule wa Sh310 bilioni wa Bandari ya Lamu (Lapsset) eneo la Kililana.
Kiegesho cha kwanza cha mizigo katika mradi huo kilifunguliwa na Rais Uhuru Kenyatta kwenye hafla iliyoandaliwa mnamo Mei 20, 2021.
Ni siku hiyo ambapo historia pia iliandikwa pale meli ya kwanza ya mizigo kwa jina MV CAP Carmel ilitia nanga kwa mara ya kwanza, kuashiria mwanzo wa biashara ya kupakua, kupakia na shughuli za uchukuzi wa meli kwenye bandari hiyo ya Lamu.
Ya pili baada ya Kilindini
Bandari ya Lamu (Lapsset) ni ya pili hapa nchini baada ya ile ya Kilindini mjini Mombasa.
Kufikia sasa, biashara ya uchukuzi wa meli imenoga Lamu na Pwani kwa jumla kwani kufikia sasa tayari jumla ya meli tisa za mizigo zimetia nanga kwenye bandari hiyo baada ya kufunguliwa kwake miezi minane iliyopita.
Mbali na MV Cap Carmel, meli nyingine zilizotia nanga bandarini Lamu ni MV Seago Bremerhaven, MV Spirit of Dubai, MV Seago Pireaus, MV Seago Istanbul, Ionian Express, MV Zuhra II na MV Amu 1 kutoka Zanzibar ambayo ilitia nanga mara mbili bandarini humo.
Meneja wa Bandari ya Lamu, Bw Abdullahi Samatar, alitaja ufunguzi wa bandari hiyo mwaka huu kuwa wa natija tele kibiashara si kwa Lamu tu bali Kenya nzima, Afrika Mashariki na ulimwenguni kwa jumla.
“Tunafurahia kufunguliwa kwa bandari ya Lamu mwaka huu. Meli kadhaa tayari zimewahi kutia nanga bandarini hapa katika kipindi hiki kifupi cha miezi minane tangu ifunguliwe. Tuko na msururu wa meli nyingine ambazo pia zimetangaza kwamba zitafika hapa kabla ya mwaka huu kukamilika. Hiyo ni ishara tosha kwamba bandari ya Lamu ni kiungo mwafaka cha kibiashara,” akasema Bw Samatar.
Mradi mwingine mkuu uliokamilika na kuanza shughuli mwaka huu ni ule wa Sh10.8 bilioni wa barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen.
Barabara hiyo ya kilomita 135 imekuwa ikijengwa tangu Machi 9, 2017, ambapo ujenzi wake ulizinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta mjini Witu.
Kampuni ya Ujenzi ya H-Young kwa ushirikiano na GIBB Africa Limited ndiyo iliyotekeleza ujenzi wa barabara hiyo ambayo ni kiunganishi cha kipekee cha Lamu na sehemu nyingine za Kenya.
Mei 20, 2021, Rais Uhuru Kenyatta alifungua rasmi mradi huo, siku hiyo hiyo ambayo alifungua rasmi shughuli za bandari ya Lamu.
Tangu kufunguliwa kwake, barabara hiyo imeshuhudia kuimarika pakubwa kwa biashara ya uchukuzi Lamu.
Idadi ya magari ya uchukuzi wa abiria yanayohudumu kwenye barabara hiyo kwa sasa imeongezeka maradufu tangu ujenzi ulipokamilika na mradi kufunguliwa na Rais Kenyatta miezi minane iliyopita.
Barabara hiyo pia imechangia pakubwa usalama, amani na utulivu kushuhudiwa Lamu kinyume na miaka ya awali ambapo wapiganaji wa al-Shabaab walikuwa wakitumia mwanya wa barabara mbovu na vichaka kushambulia, kujeruhi na hata kuua abiria na walinda usalama kwenye barabara hiyo.
Barabara ya Lami
“Tunafurahia kupata barabara mpya ya lami eneo hili. Tumevumilia kutumia barabara mbaya na vumbi tangu uhuru wa nchi hii kupatikana. Pongezi kwa serikali yetu kutujengea na kutukamilishia barabara hii,” akasema Salim Omar, mmoja wa madereva wa magari ya uchukuzi wa umma eneo hilo.
Kukamilika kwa barabara ya Lamu-Witu-Garsen pia kumeipa serikali imani, hasa kiusalama, hivyo kutangaza kuondolewa kwa marufuku ya kusafiri usiku, hasa kwa magari ya uchukuzi wa mizigo.
Marufuku hayo yalikuwa yamedumu eneo hilo tangu 2014.
“Tumeafikia kuondoa marufuku ya usiku kwa magari yanayobeba mizigo, ikiwemo vyakula, bidhaa za ujenzi, mazao ya mashambani nakadhalika. Mtanipa muda zaidi kujadiliane na kamati ya usalama eneo hili kujua iwapo tunaweza kuruhusu magari ya usafiri wa umma pia kuhudumu usiku. Nitatoa uamuzi katika kipindi cha wiki mbili zijazo,” akasema Mshirikishi wa Usalama Ukanda wa Pwani, John Elungata.
Next article
2021: Serikali yakosa kutimiza lengo la kuchanja kikamilifu…