[ad_1]
UTOVU WA NIDHAMU: Lyon na Paris FC watupwa nje ya French Cup
Na MASHIRIKA
OLYMPIQUE Lyon na Paris FC wametupwa nje ya kipute cha French Cup msimu huu baada ya mechi yao kuvurugwa na mashabiki waliozua fujo na vurumai uwanjani.
Mechi hiyo iliyoandaliwa na Paris FC mnamo Disemba 17, 2021 ilivurugwa na matukio ya fujo miongoni mwa mashabiki huku baadhi wakirusha vifaa uwanjani na kulipua fataki. Mchuano huo ulifutiliwa mbali mwishoni mwa kipindi cha kwanza matokeo yakiwa 1-1.
Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka la Ufaransa lilitoza Paris FC faini ya Sh1.3 milioni huku Lyon wakitozwa faini ya Sh6.8 milioni kwa hatia ya kukosa kudhibiti mashabiki wao wakati wa gozi hilo.
Lyon wamewahi pia kupokonywa alama katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) msimu huu baada ya mashabiki wao kuzua fujo wakati wa mechi iliyowakutanisha na Olympique Marseille.
Mechi hiyo ilisimamishwa ghafla baada ya kiungo Dimitri Payet kugongwa kichwani na chupa ya maji iliyorushwa na mmoja wa mashabiki sogora huyo wa zamani wa West Ham United alipokuwa akijiandaa kupiga mpira wa kona.
Mchuano mwingine wa Marseille dhidi ya Nice ugenini uliwahi kusimamishwa mnamo Agosti baada ya Payet kuokota chupa ya maji aliyorushiwa na kuitupa kwa mashabiki. Tukio hilo lilizua fujo na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali uwanjani baada ya mashabiki kujitoma uwanjani kwa vurugu na kumkabili visivyo kiungo Valentin Roniger wa Marseille ambaye bado anauguza majeraha.
Mechi ya Ligue 1 kati ya RC Lens na Lille mnamo Septemba iliwahi pia kucheleweshwa kwa zaidi ya dakika 30 baada ya mashabiki wa vikosi pinzani kuanza kurushiana vifaa uwanjani.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO
Next article
Mshambuliaji Hakim Ziyech atupwa nje ya kikosi…
[ad_2]
Source link