Maafisa wa serikali wanaotaka kuwania viti wana siku 30 kung’atuka – IEBC
Na CECIL ODONGO
MWENYEKITI wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) Wafula Chebukati kwa mara nyingine amesisitiza kuwa watumishi wa umma ambao wanalenga kuwania nafasi za uongozi wana siku 30 pekee kabla ya kung’atuka serikalini.
Bw Chebukati alisema kuwa watumishi hao wanaosaka cheo chochote kati ya sita vilivyoko kwenye Katiba, wana hadi Februari 9 ili kung’atuka jinsi Sheria za Uchaguzi zinazoamrisha.
Afisa huyo alisema kuwa IEBC itatumia sheria jinsi ilivyokuwa mnamo 2017 akisema mahakama haijatoa uamuzi kuhusu kesi iliyowasilishwa kupinga kung’atuka kwa maafisa hao miezi sita kabla ya uchaguzi kufanyika wakisema ni ya kibaguzi.
“Kesi kuhusu suala hili ipo mahakamani na amri ilitolewa kuwa sheria iliyotumika 2017 iendelee kutekelezwa hadi pale kesi itakaposikizwa na kuamuliwa. Mnamo Disemba 21, 2021 mahakama iliamrisha IEBC itekeleze sheria hiyo jinsi ilivyokuwa hapo awali,” akasema Bw Chebukati.
Rufaa iliyowasilishwa kuhusu kesi hiyo itatajwa mnamo Januari 24, 2022Kutokana na hilo baadhi ya mawaziri ambao wanalenga viti vya kisiasa pia watalazimika kujiuzulu kabla ya Februari 9 ili kutimiza matakwa ya sheria hiyo.
Kati ya mawaziri ambao huenda wakajiuzulu ni Peter Munya na Sicily Kariuki ambao wanalenga viti vya ugavana katika kaunti za Meru na Nyandarua.
Pia mawaziri wasaidizi, makatibu wa wizara mbalimbali na wanasiasa walioteuliwa kwenye mashirika ya serikali pia hawatasazwa kwa kuwa baadhi yao tayari wameonyesha nia ya kuwania nafasi za uongozi.
Aidha, Chebukati ambaye alikuwa akizungumza mjini Naivasha, alisema kuwa vyama 82 vya kisiasa vimetimiza masharti yote ya kisheria na sasa vitaruhusiwa kushiriki uchaguzi mkuu wa mnamo Agosti mwaka huu.
Kwa mara nyingine, Wakenya ambao hawakujisajili kama wapigakura katika mkumbo wa kwanza mwezi uliopita, sasa wana nafasi nyingine ya kujisajili, IEBC ikiratibu usajili huo uanze mnamo Januari 17 hadi Februari 6.
Katika usajili wa kati ya Oktoba 4 hadi Novemba 5 mwaka uliopita, IEBC iliwasajili wapigakura wapya milioni 1.5 dhidi ya idadi lengwa ya milioni 6.5.
“Huu utakuwa usajili wa mwisho kabla ya uchaguzi mkuu kuandaliwa. Kwa hivyo, nawaomba vijana ambao wana vitambulisho wafike kwenye vituo mbalimbali ndipo wajisajili. Kwa wale ambao hawana vitambulisho, watafute stakabadhi hiyo kwa wakati kabla hawajafungiwa nje,” akaongeza.
Mchakato huo wa usajili umefaulishwa baada ya IEBC kupokea pesa za ziada kutoka kwa Hazina ya Kitaifa ya Kifedha.
Wale wapigakura wanaoishi nchi za nje nao wataanza kusajiliwa kuanzia Januari 21 hadi Februari 6.Kando na mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Chebukati alisema wameongeza Marekani, Canada, Uingereza, Sudan Kusini, Milki ya Kiarabu na Ujerumani kwenye orodha ya nchi ambako raia watajisajili kuanzia Januari 21 hadi Februari 6.
Hata hivyo, Wakenya ambao wanaishi ng’ambo na wako nchini kwa sasa, wameshauriwa wafike katika afisi za IEBC kwenye Jumba la Annivasary Towers ili kufanya hivyo.
Next article
Majonzi watu 5 wa familia moja walioangamia ajalini…