Maandalizi ya kisasa kwa Team Kenya Jumuiya ya Madola
Na AYUMBA AYODI
KAMATI ya Kitaifa ya Olimpiki (NOC-K) inataka kikosi cha timu ya taifa ya Kenya ya michezo ya Jumuiya ya Madola 2022 ianze maandalizi mwezi Januari.
Aidha, NOC-K inataka mashirikisho yajiandae kutaja vikosi vyao vya kwanza vya kujiandaa kwa mashindano hayo yatakayofanyika mjini Birmingham.Kenya inalenga kuingiza wanamichezo 200 katika mashindano yatakayofanyika Julai 28 hadi Agosti 8.
NOC-K inalenga kufanya mazoezi ya timu za taifa kufanywa kuwa ya kisasa hata baada ya mashindano ya Birmingham.“Tunataka kufanya mazoezi ya kisasa ya michezo ya Jumuiya ya Madola ya Birmingham wakati tutatupilia mbali mazoezi ambayo tumezoea kufanya na kupea kila timu vifaa vya kisasa vinavyofaa fani zao,” alisema Katibu Mkuu wa NOC-K, Francis Mutuku.
“Tulishuhudia jinsi timu ya voliboli ilivyozamia mazoezi kwa kutumia vifaa vya kisasa. Timu ya raga ya wachezaji saba kila upande hufanya mazoezi ya kisasa na tunataka kila timu ifuate mkondo huo,” alieleza Mutuku.Aliongeza kuwa watahakikisha kuwa serikali itasambaza vifaa vya mazoezi.
“Lengo letu ni kuwa na kikosi imara na pia idadi kubwa ya wanamichezo wakati wa mashindano ya Afrika Games mwaka 2023, Olimpiki za Paris 2024 na Olimpiki za chipukizi 2026,” akasema.Katibu alifichua jana kuwa maafisa wa kuhudumu katika kamati za kuendesha na kusimamia timu ya Kenya wakiwemo Kiongozi wa msafara, watateuliwa mwezi ujao.
Kenya ilikuwa na wanamichezo 136 wakati wa Michezo ya Jumuiya ya Madola 2018 mjini Gold Coast ikivuna medali 17 (dhahabu nne, fedha saba na shaba sita).“Tunalenga angaa medali 20 zikiwemo dhahabu sita,’ alisema Mutuku na kufichua kuwa NOC-K imefanya mikutano mingi ya michezo ya Birmingham.
NOC-K imeandikia mashirikisho ya uogeleaji, riadha, badminton, ndondi, uendeshaji wa baiskeli, sarakasi, judo na miereka kuanza shughuli kuchagua vikosi vyao.Mashirikisho ambayo lazima yahudhurie mashindano ya kufuzu ni tenisi ya mezani, unyanyuaji wa uzani, voliboli ya ufukweni, voliboli, mpira wa magongo, mpira wa pete na raga ya wachezaji saba kila upande.