MIKIMBIO YA SIASA: Maangi kumhepa Ruto kuna tija gani kwake kisiasa?
Na CHARLES WASONGA
NAIBU Rais William Ruto anazidi kutorokwa na baadhi ya wanasiasa waliokuwa wandani wake sugu kando wanaojiunga na kambi ya kiongozi wa ODM Raila Odinga.
Katika siku za hivi karibuni Bw Odinga, ameendelea kuvuna uungwaji mkono katika iliyokuwa ngome ya Jubilee ya eneo la Mlima Kenya.
Hii ni kutokana na ukuruba wa kisiasa kati yake na Rais Uhuru Kenyatta.
Mwanasiasa wa hivi punde kumhepa ni Naibu Gavana wa Kisii Joash Maangi ambaye tangu 2018 amekuwa mfuasi wake mkuu wa Dkt Ruto kutoka eneo pana la Gusii.
Mnamo Desemba 10, Bw Maangi alikuwa miongoni mwa wajumbe kutoka kaunti ya Kisii waliohudhuria mkutano wa Azimio la Umoja katika uwanja wa Kasarani.
Akiongea na wanahabari katika uwanja huo, Bw Maangi alisema ni vigumu kumuuza Dkt Ruto, na chama cha United Democratic Alliance (UDA), katika eneo la Kisii kwa sababu wakazi wengi wanahusudu chama cha ODM.
“Nimeamua kurejea katika chama changu cha ODM kwa sababu watu wetu kule Kisii wamekataa katakata kukumbatia UDA. Wengi wanamhusudu Raila Odinga,” Bw Maangi akasema katika uwanja huo ambako Bw Odinga alitangaza rasmi kuwa atawania urais katika uchaguzi mkuu wa 2022.
Hatua ya Bw Maangi kuhudhuria mkutano wa Azimio la Umoja iliwashangaza watu wengi katika mitandao ya kijamii, ambao awali walimhama kama mfuasi sugu wa Dkt Ruto.
Lakini Bw Maangi alianza kuonyesha dalili ya kubadili msimamo alipokwepa kuhudhuria mikutano ya kampeni ya Dkt Ruto katika eneo la Marani, (eneobunge la Kitutu Chache Kaskazini), Nyaribari Masaba na Bobasi kaunti ya Kisii.
Aidha, Bw Maangi amekosa kuhudhuria mikutano kadha ya kampeni iliyoongozwa na Naibu Rais katika kaunti ya Nyamira tangu mwezi Novemba.
Lakini mnamo Oktoba 2021, Bw Maangi alikuwa mstari wa mbele kuisuta serikali kwa kuwanyanyasa wandani wa Dkt Ruto, akiwemo yeye, kwa kuwakamata bila sababu.
“Wagombeaji urais wengine wanazuru maeneo mbalimbali bila vikwazo. Nashangaa kuwa kampeni za Naibu Rais zimekuwa zikihujumiwa kwa fujo huku sisi kama wafuasi wake tukikamatwa,” akasema akiwa nyumbani kwake katika kijiji cha Ogembo, kaunti ndogo ya Gucha.
Bw Maangi amewahi kukamatwa hapo awali kwa kile alichodai ni kutokana na uhusiano wa kisiasa kati yake na Dkt Ruto.
Kwa mfano, mnamo Februari 15, 2021 Naibu huyo wa Gavana alikamatwa katika hali ya kutatanisha akisubiri kumpokea Dkt Ruto katika uwanja wa Shule ya Upili ya Kisii.
Naibu Rais alikuwa amepangiwa kuhudhuria mazishi ya waziri wa zamani na mwanasiasa wa haiba kubwa katika jamii ya Abagusi, Simon Nyachae.
Kabla ya kujiunga kambi ya Bw Odinga, Bw Maangi alikuwa ametangaza kuunga mkono mchakato wa marekebisho ya katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI).
Kwenye mahojiano na ukumbi huu, Bw Maangi alisema kuwa anapania kuwania ugavana wa Kisii kwa tiketi ya ODM katika uchaguzi mkuu ujao.
“Mimi ndiye kiongozi ninayefaa zaidi kuchukua hatamu za uongozo wa kaunti hii baada ya Gavana James Ongwae kukamilisha muhula wake wa pili na wa mwisho. Bila shaka hii ni mojawapo ya sababu zilizochangia hatua yangu ya kubadili msimamo wa kisiasa na kuhama mrengo wa Naibu Rais,” akaeleza.
Wadadisi wa siasa za Kisii wanasema hatua Bw Maangi kuamua kuunga mkono Bw Odinga ni pigo kubwa kwa kambi ya Dkt Ruto sio tu katika kaunti ya Kisii bali hata katika kaunti ya Kisii.