#KCPE2021: Mabingwa wafichua siri ya ufanisi wao
NA WAANDISHI WETU
BIDII, nidhamu, na ari ya kuondoa familia zao katika umaskini ni baadhi tu ya sababu zilizochangia wanafunzi kutia fora katika Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi (KCPE).
Mvulana aliyeibuka nafasi ya kwanza Pwani alitarajia kupata alama zaidi ya 421 alizopata.
Joshua Safari Ziro, ambaye alifanya mtihani wake katika Shule ya Msingi ya Busy Bee alisema wakati Waziri wa Elimu, Prof George Magoha, alipotangaza mwanafunzi wa kwanza kitaifa aliyepata alama 428, alikufa moyo.
“Ingawa nimefanya vyema, hizo si alama nilizotarajia. Nilikufa moyo niliposikia kile ambacho mwanafunzi wa kwanza kitaifa alipata lakini mamangu alinitia moyo,” akasema.
Kulingana naye, kilichomsukuma kutia bidii masomoni ni ari ya kuwa kielelezo bora kwa wadogo wake kwani ndiye kifungua mimba katika familia ya watoto watatu wa kiume.
“Nilikuwa nikilala kuchelewa usiku na katika siku nyingine, kukosa kula chakula cha mchana kusudi nipate muda wa kutosha wa kusoma darasani,” akasema.
Azimio lake ni kujiunga na Shule ya Upili ya Alliance kisha baadaye awe daktari.
Mama yake, Bi Lorraine Mlamba, alisema alimhamisha Joshua shule tatu kabla ya kujiunga na Busy Bee katika darasa la saba kwa kuwa alikuwa akiongoza kila mara katika shule za awali.
“Nilitaka awe mahali ambapo angalipata ushindani wa kimasomo. Alipofanya mahojiano ya kujiunga na shule hii, aliibuka katika nafasi ya nne na nikajua hapa ndipo anastahili kuwa,” akasema Bi Mlamba.
Sawa na Joshua, mwanafunzi aliyeibuka wa pili Pwani, Lisa Adhiambo, alitarajia kuzoa alama zaidi ya 420 alizopata. Lisa ambaye ndiye wa kwanza kati ya watahiniwa waliofanya mitihani katika shule za umma, alipita mitihani yake katika Shule ya Msingi ya Amani iliyo Mombasa, licha ya changamoto zinazokumba familia yake.
Kilichompa ari ya kutia bidii masomoni ni kuwa, hakutaka hatima ya jamaa zake wengine walioacha shule kwa sababu ya umaskini impate.
Vile vile, alifahamu fika kuwa ni kupitia kwa matokeo bora ambapo atazingatiwa kupata ufadhili wa kuendeleza masomo yake kwani ana hakika wazazi wake watatatizika kupata karo.
“Ninajivunia familia yangu licha ya umaskini unaotukumba. Ninafurahi kuwa wazazi wangu wamejitolea ili kuhakikisha nimeenda shuleni,” akasema.
Mamake, Bi Diana Akinyi, alisema binti yake hupenda kusoma lakini yeye hakutarajia angeibuka na alama hizo nyingi katika KCPE.
“Niliacha shule kwa sababu ya kukosa karo na nisingelipenda binti yangu apitie hali sawa na hiyo. Mume wangu hufanya kibarua Nairobi na mimi ni mke nyumbani lakini tumefurahi kwamba Lisa ametufanya tung’ae,” akasema.
Katika Kaunti ya Kilifi, Kelly Bar – aka aliyepata alama 420 kutoka shule ya msingi ya Almona Junior Academy iliyo Malindi, alisema juhudi za walimu na wazazi kumkuza katika mazingira bora zilimuwezesha kufanya vyema masomoni.
“Kwa yote namshukuru Mungu kwa kunisaidia. Na pia nawashukuru walimu wangu kwa kunisaidia katika masomo yangu hasa katika yale masomo yaliyokuwa yakinitatiza. Wamekuwa mstari wa mbele kunihimiza nitie bidii zaidi na nitakuja kufaulu na saa hii nafurahia kwa kuwa nimepata hizo alama,” akasema.
Kelly angependa kujiunga na Shule ya Upili ya Alliance akitaka kutimiza ndoto ya kuwa mhandisi. Mama yake, Bi Elvina Faida alisema nidhamu aliyokuzwa nayo mtoto huyo imechangia kufaulu kwake.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bw Jared Otieno, alisema licha ya kuwa na muda mfupi wa
kusoma kwa wanafunzi kufuatia janga la corona walijitahidi katika kuwatayarisha vyema ili kuhakikisha wanafaulu.
Katika Kaunti ya Lamu, Al- Amin Mahamoud Mohamed Ahmed ameandikisha historia kwa kuwa wa kwanza kuwahi kupata zaidi ya alama 400 (KCPE) katika Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki.
Mwanafunzi huyo aliyefanya KCPE katika shule ya msingi ya wavulana ya Kizingitini ambayo ni ya umma, alipata alama 403.
Al-Amin alitaja hali ngumu ya maisha na ufukara unaomkumba mamake na familia kwa jumla kuwa kigezo kilichomsukuma kutia bidii maishani.
“Nitaendelea kusoma kwa bidii ili kuiokoa familia yetu. Nataka mamangu awe mahali pazuri punde nikihitimu masomo yangu, niwe rubani. Mamangu amenipigania sana kuona kwamba ninafaulu maishani,” akasema.
Mama YAke, Bi Muhsina Vae anasema atajitolea kwa hali na mali kuhakikisha mwanawe anatimiza ndoto yake ya kuwa rubani.
“Mimi sina kazi lakini nimehakikisha heri nilale njaa lakini mwanangu awe na kila rasilimali ya kumfanya asome na kupita mitihanini. Nilijua fika kuwa sina cha kumrithisha mwanangu isipokuwa elimu,” akasema Bi Muhsina.
Ripoti za Farhiya Hussein, Brian Ocharo, Winnie Atieno, Alex Kalama na Kalume Kazungu
Next article
Vyama huru kutoa tiketi bila mchujo