SHINA LA UHAI: Maelfu ya Wakenya wakabiliwa na uziwi ukubwani
LEONARD ONYANGO Na WANGU KANURI
JAPO baadhi ya watu huzaliwa wakiwa na tatizo la kusikia vyema, wengi hukumbwa na uziwi ukubwani.
Wataalamu wanasema wengi wa watoto wanaozaliwa wakiwa na tatizo la kusikia vyema baadaye huwa viziwi kutokana na hatua ya wazazi kuchelewa kuwapeleka hospitalini kupata matibabu.
“Visa vingi vya uziwi vinaweza kuzuilika iwapo vitatambuliwa mapema baada ya mtoto kuzaliwa na kutibiwa. Kuchelewesha matibabu ndiko kumechangia kuwepo kwa visa vingi vya uziwi,” anasema Dkt Njoroge Muhuhu, mtaalamu wa afya jijini Nairobi.
Anasema kuwa mtoto anapozaliwa anafaa kufanyiwa vipimo ili kubaini ikiwa masikio yako sawa au la kabla ya kuondoka hospitalini.
Lakini kinachoshtua wataalamu zaidi ni ongezeko la watu wazima wanaopatwa na uziwi au matatizo ya kusikia humu nchini.
Wataalamu wanasema kuwa uziwi huo unasababishwa na kuwa kwenye mazingira yenye kelele nyingi kwa muda mrefu hasa kutokana na magari, maeneo ya burudani au kusikiliza muziki wa juu kwenye matatu au nyumbani.
Ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (Unep) inaonyesha kuwa wastani wa kelele jijini Nairobi, ni zaidi ya kiwango kinachopendekezwa na Shirika la Afya Duniani-WHO.
Shirika la WHO, linapendekeza kuwa wastani wa kelele mchana unafaa kuwa chini ya 60 decibels (dB) na usiku chini ya 50 dB. Decibels ni kipimo ambacho hutumika kupima kiwango cha kelele katika eneo fulani.
Lakini ripoti ya 2022 kuhusu kelele inaonyesha kuwa wastani wa kelele jijini Nairobi ni zaidi ya 70 dB – kumaanisha kuwa wengi wa wakazi wako katika hatari ya kukumbwa na shida ya kusikia.
Kulingana na WHO, mtu akikaa kwenye mazingira ya kelele ya kati ya 90 na 100 dB – ambayo ni sawa na mlio ambao hutolewa na gari la ambulansi – kwa dakika 15 kwa siku, anaanza kukabiliwa na tatizo la kusikia.
Kelele inayosababishwa na mvua juu ya mabati pia inaweza kusababisha uziwi kwa mujibu wa WHO.
Vijana wapiga gumzo huku wakisikiliza muziki wakiwa katika matatu ya Rongai (Nambari 125) Januari 28, 2016. PICHA | MAKTABA
Watu ambao huathiriwa zaidi na kelele, haswa wakati wa usiku, ni kina mama wajawazito na watu wazee, kwa mujibu wa WHO.
Mtu akigutushwa kwa kelele akiwa amelala anaweza kukumbwa na tatizo la msongo wa mawazo na kutatiza jinsi mwili hufanya kazi. Hii ni kwa sababu usingizi ni muhimu katika kudhibiti mapigo ya moyo na kusambaza sukari mwilini.
WHO linaonya kuwa watu wanaoshindwa kulala vyema kutokana na kelele wanakuwa katika hatari ya kupata magonjwa ya moyo, kisukari na hata shinikizo la damu.
Mazingira yenye utulivu hufanya akili kupumzika vyema na hivyo kuepuka matatizo hayo ya kiafya.
Nchini Kenya, mtu mmoja kati ya kumi hutatizika kusikia huku WHO likikadiria kuwa kati ya vijana wawili, mmoja huathiriwa na kelele.
“Ulemavu wa kusikia ni mojawapo ya ulemavu ambao tunaweza zuia,” anasema Dkt Lilian Mokoh, mtaalamu wa magonjwa ya Masikio, Pua na Koo (ENT).
“Uziwi kwa vijana hutokana na vifaa vya kusikiza muziki, vilabu na matatu yenye muziki wa juu al-maarufu nganya,” anaeleza Dkt Mokoh.
Dkt Nancy Kemunto, mtaalamu wa Afya ya Masikio anasema kuwa afya ya masikio inaweza kuzingatiwa kwa kupangusa sehemu ya nje kwa kitambaa.
“Kuingiza kile kijiti chenye pamba ndani ya masikio ili kutoa nta kunaweza ziba sikio. Masikio hujiosha yenyewe,” afafanua Dkt Kemunto.
Aidha Dkt Mokoh anashauri kuwa mtu anaweza jua kuwa masikio yake yameathirika iwapo anasikia kwenye sikio lake moja kelele kama ya kengele yenye sauti ya juu.
Vile vile iwapo mtu hasikii sauti kikamilifu, ama anahisi ni kama ana maji kwenye masikio, basi hiyo ni ishara kuna haja kusaka matibabu.
Mwaka huu katika maadhimisho ya Siku ya Kusikia Duniani, kauli mbiu ya WHO ilikuwa, ‘Ili kusikia maishani, sikiliza kwa makini.’
“Duniani, zaidi ya watu bilioni 1.5 hutatizika kusikia huku aghalabu watu milioni 430 na watoto milioni 34 wakihitaji usaidizi wa kiafya. Isitoshe, zaidi ya watu asilimia 5 duniani huishi na matatizo ya kusikia,” lasema WHO
Aidha, WHO linakadiria kuwa ifikapo 2050, watu bilioni 2.5 watakuwa wanashindwa kusikia kwa kiwango na angalau wengine milioni 700 watakuwa wanasaidiwa ili kuweza kusikia tena.
Duniani, nusura vijana asilimia 50 kati ya miaka 12 na 35 wapo kwenye hatari ya kupoteza uwezo wao wa kusikia. Vijana hao bilioni 1.1 wanaathiriwa sababu ya muziki wa sauti ya juu.
WHO linaonya kwamba idadi ya Wakenya wanaokumbwa na tatizo la kusikia imeendelea kuongezeka ikilinganishwa na idadi za kimataifa ambazo ni watu watano kwa kila watu 100.
Wataalam wanahoji kwamba matatizo mengi yanayoathiri uwezo wa kusikia na hatimaye kusababisha uziwi hapa Kenya, yanaweza kabiliwa endapo vifaa na huduma muhimu zitaimarishwa.
Gharama
Lakini miongoni mwa wagonjwa 30 wanaohitaji vifaa hivyo vya kuongeza uwezo wa kusikia, ni watano pekee wanaoweza kulipia kutoka mifukoni mwao.
Gharama ya juu ya kutibu masikio humu nchini, hufanya Wakenya wengi kushindwa kutafuta huduma za matibabu.
Kwa mfano, vifaa vya kusaidia mwathiriwa kusikia vinagharimu Sh50,000 huku kuwekewa vifaa vya kusikia masikioni kwa njia ya upasuaji kukigharimu zaidi ya Sh2.5 milioni.