Mahangaiko zaidi Miguna akijaribu kurejea nchini
Na RICHARD MUNGUTI
SAFARI ya kurudi nyumbani ya wakili na mwanaharakati mbishi Dkt Miguna Miguna ilikumbwa na mawimbi pale ubalozi wa Kenya Berlin ulipokawia kumpa stakabadhi.
Kufuatia tukio hilo, Dkt Miguna Jumatatu alidai kwamba Ubalozi wa Kenya nchini Ujerumani ulimnyima stakabadhi za usafiri licha ya agizo la mahakama kuu.
Kwenye ujumbe alioweka katika mtandao wa Twitter, Dkt Miguna alisema Balozi wa Kenya Tom Amolo alitoroka punde tu alipowasili afisini mwake.
Alidai Bw Amolo aliwaambia wafanyakazi wa ubalozi huo -Bi Emmah Mabinda, Bw Kaluma na Bi Esther Mungai- wangepoteza kazi zao ikiwa watampa stabadhi za usafiri ilivyoagizwa na mahakama.
Alisema Bi Mabinda alimweleza hajapokea maagizo kutoka Nairobi kutekeleza maagizo ya mahakama.
“Alinitaka kudhihirisha Uraia Wangu ndipo nikamwonyesha kitambulisho changu kisha akaniitisha cheti cha kurejeshewa uraia,” Dkt Miguna alidokeza.
Awali mahakama kuu iliamuru ubalozi huo umpe stakabadhi za usafiri.
Jaji Hedwiq Ong’udi alimtaka Bw Miguna apate Visa kutoka Ubalozi wa Kenya katika muda wa masaa 72 ili akubaliwe kuabiri ndege itakayo safari kutoka Berlin, Ujerumani hadi Nairobi.
Mahakama iliamuru shirika la Ndege la Air France imsafirishe Miguna hadi Nairobi akiikabidhi hati hali za kusafiria.
Na wakati huo huo Jaji Ong’udi aliamuru Waziri wa mashauri ya nchi za
Kigeni Bi Rachel Omamo ahakikishe agizo hilo la kumruhusu Miguna kurudi nchini imetekelezwa.
Akitoa uamuzi katika ombi la Bw Miguna, Jaji Ong’udi alisema Bw Miguna yuko na uraia wa nchi mbili na anatakiwa kupata Visa ili aruhusiwe kusafiri kurudi Kenya.
Akitoa uamuzi Jaji Ong’udi alisema,“nimezingatia ushahidi wote uliowasilishwa na mawakili wa mlalamishi (miguna).Namwamuru mlalamishi apate Visa kutoka kwa Ubalozi wa Kenya nchini Berlin ili aruhusiwe kuabiri ndege kurudi Kenya.Yeye yuko na uraia wa nchi mbili Kenya na Canada.”
Punde tu alipofahamishwa na mawakili Nelson Havi na Dkt John Khaminwa kuhusu uamuzi wa mahakama kuu Bw Miguna alichapisha ujumbe katika mtandao wake wa Twitter na kusema ”Sitatembelea Ubalozi wa Kenya mjini kuomba Uraia ambao sikuupoteza. Mahakama imethibitisha tena kwamba mimi ni raia wa Kenya na ninapasa kurudi Kenya nikutumia kitambulisho changu cha kitaifa. Ubalozi wa Kenya umeagizwa na Mahakama kuu unipe cheti cha kusafiria-Miguna Miguna.”
Baada ya muda mdogo, Dkt Miguna alichapisha ujumbe mwingine akiwapongeza mawakili Nelson Havi na Dkt Khaminwa kwa kupata maagizo hayo.
Hata hivyo alibadili nia na kusema atafululiza hadi afisi ya Ubalozi wa Kenya mjini Berlin katika muda wa masaa mawili kupata cheti cha kumwezesha asafiri kurudi Kenya.
Dkt Miguna alifurushwa kutoka nchini Kenya 2018 baada ya kumwamipisha aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kuwa “rais wa watu”
Mawakili Havi na Dkt Khaminwa waliwasilisha kesi wakiomba mahakama kuu ishurutishe Serikali kumruhusu Bw Miguna arudi nchini. Mwaka wa 2018 Dkt Miguna alifurushwa kutoka nchini.
Kabla ya kuvurushwa nchini 2018 mahakama kuu ilikuwa imeamuru,Bw Miguna afikishwe kortini polisi wakakaidi agizo hilo.
Jaji Enock Chacha Mwita aliamuru Serikali imlipe Dkt Miguna fidia ya Sh7.2milioni. Na wakati huo huo mahakama ikamtoza faini ya Sh200,000 Waziri wa Usalama Dkt Fred Matiang’i kwa kukaidi agizo Dkt Miguna afikishwe kortini. Mahakama iliamuru pesa hizo zitolewe kwa mshahara wa Dkt Matiang’i.