MAKALA MAALUM: Maiti za wanyonge kuzikwa na NMS bila jamaa zao kujua
DAN OGETTA Na ANGELINE OCHIENG’
BAADHI ya familia ambazo wapendwa wao wapo kwenye orodha ya karibu miili 500 iliyotolewa na Shirika la Huduma za Jiji (NMS) ili kuzikwa kwenye makaburi ya pamoja, hazifahamu kuwa wanafamilia wao walipoteza maisha yao.
NMS ilitoa orodha hiyo ikisema kuwa ilikuwa inapanga kuizika miili hiyo iwapo wapendwa wao hawangejitokeza kuichukua. Miili hiyo iliyohifadhiwa kwa zaidi ya miezi sita ipo katika vyumba vya kuhifadhi maiti vya City na hospitali za Mama Lucy na Kenyatta.
Taifa Leo ilipotembelea familia za baadhi ya wafu hao, hawakuwa na habari kuwa wapendwa wao waliaga dunia miezi sita iliyopita huku wakipiga nduru na kuzama kwenye ukiwa baada ya kupokea habari hizo za tanzia.
Katika kijiji cha Kivindu, Kaunti ya Machakos, familia ya marehemu Damaris Kanini Mutua haina habari kuwa dada yao huyo alikuwa amefariki.
Nduguye Ndambuki Mutua ndiye amebaki katika familia hiyo ya watoto watano baada ya baba yao kufariki miaka mitano iliyopita, miezi michache pia baada ya kifo cha kitindamimba wao.
Bw Mutua alisema kuwa baada ya kifo cha mama yao miaka ya 90, familia hiyo ilitengana na wakati huo Bi Damaris alikuwa katika Darasa la Sita.
Baada ya mazishi ya mama yao kila mwanafamilia alienda zake na Bw Mutua anakumbuka kuwa alizungumza na dadake mara ya mwisho miaka hiyo ya 90.
Wakati huo, Bi Damaris alimweleza kuwa alikuwa akiishi katika mtaa wa Mukuru kwa Reben. Hata hivyo, anafafanua kuwa kabla hajafa, babake alitaka sana kumwona Damaris ambaye ni msichana wake wa kwanza lakini juhudi za kumtafuta hazikuzaa matunda wakati huo.
Baada ya kupokea taarifa ya kifo cha dadake, Bw Mutua aliyeonekana kuzama kwenye lindi la fikira kutokana na ukiwa uliomjaa, alishangaza akisema kuwa hawezi kumzika dadake kutokana na umaskini mkubwa uliomlemea.
“Iwapo kuna bili yoyote ya mochari tutahitajika kulipa, basi maoni yangu ni kuwa azikwe kwenye kaburi la pamoja na miili mingine. Jinsi mnavyoona sina mali yoyote ambayo naweza kuuza kugharimia bili hiyo na pia kusafirisha maiti yake nyumbani. Sina pesa na uwezo wa kujikimu,” akasema Bw Mutua.
Katika kijiji cha Ng’alalya, Ngiini, kaunti hiyo hiyo ya Machakos, familia ya Kennedy Thiong’o haina habari kuhusu kifo chake.
Marehmu aliondoka nyumbani katikati ya mwaka 2021 akiwa amejawa na msongo wa mawazo baada ya kutalikiana na mkewe ambaye alimwacha na mtoto wao mwenye umri wa miaka miwili pekee.
Marehemu Kennedy Thiongo katika picha ya awali ambayo nayo ilipigwa upya kwa ajili ya makala haya mnamo Machi 18, 2022. PICHA | FRANCIS NDERITU
Kutokana na mahangaiko tele, alizamia uraibu wa pombe. Taifa Leo ilipofika kwenye boma lao, mamake Nancy Wanjiku alikuwa ameketi kwenye kivuli cha nyumba yake kuepuka miale kali ya jua.
Bi Wanjiku alipiga nduru baada ya kufahamishwa kuhusu mauti ya Bw Thiong’o huku akizama kwenye huzuni mkubwa na kukemea kifo kwa kumyakua mwanawe mapema.
Nduguye Charles Mimi, 42 anasema kuwa imechukua muda tangu wasikie kutoka kwa mpendwa wao ambaye hapo awali alikuwa akiwapigia simu mara kwa mara kuwajulia hali.
Jijini Nairob alikuwa akifanya kazi kama utingo kwenye magari ya usafiri ya Forward Travellers ambayo husafirisha kutoka jijini hadi mitaa ya Eastlands kama Kayole, Umoja, Komarok, Makadara na mitaa mingine.
“Tulidhani kuwa angerejea nyumbani siku moja hadi sasa ambapo mnatuambia kuwa alifariki na mwili wake upo katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Mama Lucy,” akasema Bw Mimi akibubujikwa na machozi.
Hali ni hiyo hiyo kwa familia ya Michael Oduor Okoth katika Kaunti ya Siaya.
Kwa mujibu wa mamake marehemu Okoth, Bi Rose Akinyi, ambaye ni mjane, mwanawe aliondoka nyumbani miaka 10 iliyopita ili kuja kuishi na mjombake kusaka ajira baada ya kumaliza masomo ya shule ya upili.
Mnamo Agosti 31, 2021, alipokea simu kutoka kwa mtu ambaye hakujitambulisha aliyemweleza kuwa mwanawe alikuwa ametoweka. Tangu wakati huo wamekuwa wakimtafuta bila mafanikio yoyote kabla ya kufahamishwa na Taifa Leo Jumatano kuwa mwanawe alikuwa kati ya miili ambayo NMS inapanga kuizika katika kaburi la sahau.
Kinaya ni kuwa walikuwa wametafuta mwili wake katika hospitali za Mama Lucy, Kenyatta na City bila mafanikio yoyote.
Kupatikana kwake ni afueni kwa familia hiyo kwa kuwa kulingana na tamaduni na mila ya jamii ya Waluo ni mwiko kwa mja kuzikwa nje.
“Mila yetu inaamrisha kuwa mtu akifa, lazima azikwe nyumbani. Nimefurahi kuwa mwili wake umepatikana na kuwa sasa tutampa mazishi ya heshima hapa nyumbani,” akasema ndugu yake aliyejitambulisha kama Bw Odongo.
Hata hivyo, NMS inasisitiza kuwa familia hizo zitalazimika kulipa zaidi ya Sh120,000 kabla ya kupewa miili ya wapendwa wao huku pia gharama ya kuhifadhiwa kwa miili hiyo kwenye mochari ikiwa Sh500 kila siku.
Cha kusikitisha ni kuwa bili hiyo inaendelea kupanda jinsi wanavyochelewa kuchukua miili hiyo huku NMS nayo ikitafuta amri ya mahakama kuizika kwenye kaburi la pamoja iwapo familia zao hazitaichukua.
Famili hizo sasa zinaiomba serikali iingilie kati na kufuta gharama ambazo NMS inadai. Ombi lao ni kuwa wapewe miili ya wapendwa wao waizike kwa heshima kwa kuwa huo ndio ubinadamu na jinsi mila inavyoamrisha.
Benson Kamande katika hii picha ya 2002 kabla afariki. PICHA | FRANCIS NDERITU