Maji tele Pwani lakini nyumba zakosa tone!
Na WAANDISHI WETU
MAELFU ya wakazi wa kaunti za Pwani wanazidi kutatizika kwa uhaba wa maji ambao umedumu kwa miaka mingi bila suluhisho kupatikana.
Kulikuwa na matarajio kuwa, utawala wa serikali za kaunti ungeleta suluhisho la kudumu kwa tatizo hilo sugu lakini miaka kumi baada ya ugatuzi, wengi wangali wanategemea maji ambayo si salama kwa afya.
Katika Kaunti ya Mombasa, kiwango cha maji safi ambacho hupatikana kutoka kwa kaunti jirani ni kidogo mno huku idadi ya watu na makao ikizidi kuongezeka.Zaidi ya hayo, mabomba ambayo hutegemewa kusafirisha maji hayo kwa watu wachache waliobahatika ni kuukuu ambayo hupasuka mara kwa mara.
Katika mitaa ya mabanda ambayo ndiyo huathirika zaidi, wakazi hulazimika kununua maji safi kwa bei ghali kutoka kwa wachuuzi au wategemee misaada kutoka kwa wasamaria kama vile mashirika na misikiti ambayo hujitolea kusambaza maji bila malipo.
Mpango wa serikali ya kaunti kuanzisha mradi wa kusafisha maji ya baharini ili yawe salama kwa matumizi ya nyumbani ulikwama.Mpango huo ulikuwa umepigwa jeki miaka miwili iliyopita wakati Rais Uhuru Kenyata alipoidhinisha zaidi ya ekari kumi za ardhi ya Shule ya Upili ya Shimo la Tewa kutumiwa kwa ujenzi wa kiwanda ambacho kingegharimu Sh16 bilioni.
Hata hivyo, maafisa katika kaunti walidai kuwa, ukiritimba ndani ya serikali kuu ulitatiza utekelezaji wa mpango huo.Waziri wa Maji, Bi Sicily Kariuki, alitetea wizara yake na kusema mapendekezo kuhusu mradi huo bado yanachunguzwa.
“Huu mpango uliletwa kwetu kupitia kwa pendekezo la kibinafsi. Bado linachunguzwa na Wizara ya Fedha kisha tutashauriwa kuhusu mwelekeo tunaofaa kuchukua,” Bi Kariuki alisema mwezi uliopita.
Waziri wa Fedha katika Kaunti ya Mombasa, Bi Mariam Mbaruk, alisema wana matumaini serikali itaidhinisha mpango huo kabla utawala wa Gavana Hassan Joho ukamilishe kipindi chake.Katika kaunti jirani ya Kilifi, sehemu za Magarini, Ganze na Kaloleni ni baadhi ya maeneo ambayo wakazi wamekuwa wakitaabika.
Masaibu yao yamezidishwa na mabadiliko ya tabianchi ambayo husababisha kiangazi cha muda mrefu, na kukausha mito ambayo ingewasaidia.Hali hii imewasukuma wakazi katika Kaunti Ndogo ya Magarini kuamua kuanza kuchangisha Sh200 kila mmoja, ili watafute jinsi watakavyoweza kugharamia ada za kuvutiwa mifereji ya maji karibu na vijiji vyao.
Bi Selina Maitha, kutoka kijiji cha Kakuhani, Wadi ya Garashi, alisema wanakijiji hawajapokea maji safi kwa takriban miongo miwili sasa.“Katika kijiji hiki, wanakijiji hutembea hadi kilomita 15 kutafuta maji safi.
Watu wengi hapa ni maskini kwa hivyo si rahisi kumwomba mtu achangishe pesa ilhali hana hata za kulisha watoto wake,” akasema.Ilibainika kuwa, mifereji iliyowekwa na Serikali ya Kaunti kwa minajili ya kuvuta maji kutoka Baricho, imekauka.Wanaume walilalamika kuwa hali hii imeanza kutatiza mahusiano ya kinyumbani.
“Tuna hasira kwa sababu wake zetu wanatumia muda mwingi kutafuta maji na wakirudi nyumbani huwa wamechoka. Viongozi wanafaa kuwajibika kuhakikisha wananchi wana maji safi kila mara,” akasema Bw Zinga Charo.
Waziri wa maji wa Serikali ya Kaunti ya Kilifi, Bw Kiringi Mwachitu, aliisema serikali iko mbioni kuona tatizo hilo linashughulikiwa kwa haraka.Baadhi ya wakazi katika eneo la Kibaokiche, Kaunti Ndogo ya Kaloleni, walidai kuwa maafisa wa mashirika ya kusambaza maji husababisha uhaba kusudi ili kufaidisha wachuuzi wa maji.
“Tumegeuzwa ombaomba wa maji kwa muda mrefu na sasa tumechoka na tuna hasira. Tunakunywa maji ya chumvi kutoka kwa visima. Hatupati maji safi kwa vile mifereji imekauka kwa sababu watu wachache wanataka kujinufaisha,” alisema Bw Jimmy Tomboko, mmoja wa wakazi.
Wizara ya maji imekuwa ikikagua miradi ya kujenga mabwawa kama vile ya Mwache na Makamini, Kaunti ya Kwale, ambayo yatakapokamilika yanatarajiwa yatatumiwa kusambaza maji kwa kaunti nyingine za Pwani.Ripoti za Alex Kalama, Kalume Kazungu, Winnie Atieno, Maureen Ongala na Siago Cece
kando na eneo hilo.Wizara hiyo imenuia pia kuboresha usambazaji maji kutoka kwa mabomba ya Baricho, Mzima, Marere na Tiwi.Katika Kaunti ya Lamu, baadhi ya wakazi hutegemea maji kutoka kwa visima ambayo wanasema imechangia watoto kuugua maradhi ya kuendesha, kutapika, kichocho na pia maradhi ya ngozi.
“Maji yenyewe ni tope tu. Tunayatumia bila kunyunyiziwa dawa. Tunahofia maradhi zaidi,” akasema Bi Fatma Gobu, mkazi wa Kiangwe.Tatizo sawa na hili hushuhudiwa pia katika sehemu za Kaunti za Tana River, Taita Taveta na Kwale.
Next article
Gavana Kiraitu aanza rasmi kampeni za 2022