Makueni yapinga agizo Taveta itoze kodi Mtito
Na PHILIP MUYANGA
SERIKALI ya Kaunti ya Makueni, imepinga agizo la mahakama ambalo liliipa Serikali ya Kaunti ya Taita Taveta mamlaka ya kutoza kodi za biashara mjini Mtito Andei.
Kaunti ya Makueni imedai kuwa, mahakama ilipewa habari za kupotosha ndipo ikashawishika kutoa agizo hilo.Agizo hilo lilitolewa kufuatia ombi la mwanaharakati Okiya Omtatah ambaye anataka mahakama iagize Bunge la Taifa na Seneti kuteua tume huru ya kutatua mzozo wa mipaka kati ya Kaunti za Taita Taveta, Kwale na Makueni.
Mawakili wa Makueni wameambia mahakama kuwa, Bw Omtatah alipotosha mahakama kuhusu hali ilivyo.“Mlalamishi alipotosha mahakama hii kuamini kuwa baraza la mji wa Taita Taveta lililokuwepo kabla serikali ya kaunti, lilikuwa na mamlaka ya kutoza kodi na kupeana leseni za kibiashara mjini Mtito Andei,” wakasema mawakili hao.
Kulingana na Kaunti ya Makueni, baraza la mji wa Mtito Andei ndilo lililokuwa na mamlaka ya kupeana leseni za biashara na kutoza kodi katika mji huo kabla serikali za kaunti kubuniwa.Katika hati yake ya kiapo, Msimamizi wa Kaunti Ndogo ya Kibwezi Mashariki, Bw Thomas Tuta, alisema wakazi wa Mtito Andei huwa hawatozwi kodi mara mbili jinsi ilivyodaiwa na mlalamishi.
“Mlalamishi hajawasilisha ushahidi wowote wa kuthibitisha huduma zozote ambazo Serikali ya Kaunti ya Taita Taveta hutolea wakazi wa mji wa Mtito Andei hadi kaunti hiyo iwe na mamlaka ya kukusanya kodi na mapato,” akasema Bw Tuta.
Kulingana naye, agizo kuwa Taita Taveta ikusanye kodi na kupeana leseni za kibiashara si haki ikiwa haitoi huduma zozote kwa wakazi wa mji huo.Serikali ya Kaunti ya Makueni imeomba mahakama iondoe agizo lililoipa Kaunti ya Taita Taveta mamlaka hayo, hadi wakati malalamishi haya mapya yatakaposikilizwa na kuamuliwa.
Wiki chache zilizopita, Jaji Lucas Naikuni aliagiza Serikali ya Kaunti ya Taita Taveta pekee ndiyo iwe ikitoa leseni za kibiashara na kutoza kodi katika miji ya Mackinon na Mtito Andei, na akaongeza muda wa kutekelezwa kwa agizo hilo Jumatano.
Aliambia kaunti hiyo kuwa pesa zote zitakazokusanywa ziwekwe katika akaunti ya benki itakayofunguliwa kwa pamoja na Serikali ya Kaunti ya Kwale na Makueni, ambazo zinazozania usimamizi wa miji hiyo.
Mwanasheria Mkuu, Seneti na Serikali ya Kaunti ya Makueni pia zimewasilisha ilani za kutaka kupinga mamlaka ya mahakama kusikiliza aina hiyo ya kesi.Kulingana na stakabadhi zilizowasilishwa mahakamani, mizozo hiyo imesababisha wafanyabiashara kulazimishwa kulipa kodi mara mbili kwa kaunti tofauti kwa vile hawajui kaunti gani inastahili kusimamia miji hiyo.
Bw Omtatah anataka mahakama iagize Bunge la Kitaifa na Seneti kuunda tume huru ya kutatua mizozo hiyo kabla miezi mitatu ipite baada ya agizo hilo kutolewa. Kesi itatajwa Desemba 1.