Manchester City itashiriki katika kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao baada ya marufuku yao ya miaka miwili kufutwa na mahakama ya rufaa.
Mahakama ya Kusikiza Kesi za Michezo (CAS), iliondolea klabu hiyo mashtaka ya kuvunja sheria za kudhibiti fedha inazotumia kutoka kwa udhamini kipindi cha mwaka 2012 na 2016.
Kesi hiyo ilisikizwa mnamo Juni kupitia video kabla ya uamuzi kutolewa Jumatatu, Julai 13.
“Uefa imetambua uamuzi uliofanywa na Mahakama ya Kusikiza Kesi za Michezo kupunguza faini iliyotozwa Manchester City FC na Bodi ya Kusimamia Fedha ya Uefa kwa kukiuka sheria za bodi hiyo,”
“Uefa imetambua kuwa jopo la CAS halikupata ushahidi wa kutosha ya kushikilia uamuzi wa CFCB katika kesi hii ambayo huenda madai hayo yalitokea kutokana na muda wa miaka 5 ya sheria za Uefa,” ilisoma taarifa.
Uamuz huo unatazamiwa kuwapiga City jeki katika kivumbi cha vilabu nne bora, huku mahasidi wao wakipigania tiketi ya kushiriki mtanange huo.
Chelsea, Man United na Leicester City ni miongoni mwa timu ambazo ziko mbioni kupata nafasi katika mashindano hayo ya Bara Uropa.
Kikosi cha Pep Guardiola tayari kina uhakika wa kumaliza miongoni mwa vilabu bora Ligi Kuu msimu huu na wanaweza kuongeza Kombe la FA na UEFA licha ya kupoteza taji ya nyumbani.