16-BORA UEFA: Man-United kukwaruzana na Atletico nayo Real Madrid iikabili PSG
Na MASHIRIKA
MANCHESTER United watakuwa na kibarua kizito cha kusonga mbele kwenye kampeni za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu baada ya kutiwa katika zizi moja na Atletico Madrid ya Uhispania katika raundi ya 16-bora.
Real Madrid ambao ni wafalme mara 13 wa UEFA pia watakuwa na mtihani mgumu dhidi ya Paris Saint-Germain (PSG) kutoka Ufaransa.
Fowadi wa Real Madrid Karim Benzema. PICHA | AFP
Sawa na Manchester City ya kocha Pep Guardiola, PSG wanaojivunia huduma za masupastaa Lionel Messi, Neymar Jr na Kylian Mbappe pia wanawania ubingwa wa UEFA kwa mara ya kwanza katika historia.
Chelsea ilipepeta Man-City 1-0 kwenye fainali ya msimu jana jijini Porto, Ureno. Mabingwa hao watetezi sasa watamenyana na miamba wa Ufaransa, Lille.
‘Kosa la kiufundi’ lililazimisha droo ya kivumbi hicho kurudiwa baada ya ile ya awali iliyokuwa ikutanishe PSG na Man-United; kisha Atletico na Bayern Munich kufutiliwa mbali na vinara wa Uefa.
Washikilizi wa taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Man-City watavaana na Sporting Lisbon ya Ureno nao wafalme mara sita wa UEFA, Liverpool, wakwaruzane na Inter Milan ambao ni washindi mara sita wa kombe hilo.
Katika droo ya awali, Man-United walikuwa wametiwa kwenye tapo moja na Villarreal – jambo ambalo halikustahili ikizingatiwa kwamba walikuwa wamekutana kwenye hatua ya makundi. Vinara wa Uefa walibaini kuwa teknolojia ingezuia kosa hilo kufanyika.
Straika wa Juventus Paulo Dybala. PICHA | AFP
Villarreal waliotawazwa mabingwa wa Europa League msimu uliopita watamenyana na Juventus ya Italia, RB Salzburg ya Austria ionane na Bayern, nao Benfica wachuane na Ajax kutoka Uholanzi.
Fowadi wa Bayern Munich Robert Lewandowski asherehekea baada ya kufunga bao wakati wa mechi ya Kundi E la Klabu Bingwa Ulaya ambapo FC Bayern Munich ilikwaana na FC Dynamo Kyiv mjini Munich, Ujerumani, Septemba 29, 2021. PICHA | AFP
Mechi za mkondo wa kwanza katika hatua ya 16-bora muhula huu zitasakatwa kati ya Februari 15, 16, 22 na 23 huku marudiano yakiandaliwa Machi 8, 9, 15 na 16.
Chelsea ndicho kikosi cha pekee cha EPL kitakachoanza kampeni za raundi hiyo nyumbani. Wawakilishi wengine watatu wa soka ya Uingereza wataanzia ugenini baada ya kutawala vilele vya makundi yao.
Tofauti na misimu ya awali, kanuni ya bao la ugenini haitazingatiwa muhula huu. Hivyo, vikosi vitakavyotoshana nguvu baada ya kukamilika kwa mikondo miwili vitaingia muda wa ziada. Penalti zitapigwa iwapo mshindi hatakuwa amepatikana baada ya dakika 30 za ziada.
Fainali ya UEFA msimu huu itaandaliwa jijini St Petersburg, Urusi mnamo Mei 28, 2022.