Connect with us

General News

Mapendekezo ya jopokazi kuhusu boda yatekelezwe – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Mapendekezo ya jopokazi kuhusu boda yatekelezwe – Taifa Leo

CHARLES WASONGA: Mapendekezo ya jopokazi kuhusu boda yatekelezwe

NA CHARLES WASONGA

BAADA ya serikali kusitisha msako dhidi ya wahudumu wa bodaboda wasiozingatia sheria, sasa ni wakati mwafaka kwa asasi husika za serikali kufanikisha mageuzi katika sekta hiyo.

Huu ni wakati wa serikali pamoja na wadau wengine katika sekta hiyo kuhakikisha kuwa pikipiki hizi zinazotumika katika uchukuzi wa abiria zinasajiliwa rasmi.

Usajili huu utawezesha kutambuliwa kwazo ili iwe rahisi kwa walinda usalama kuzinasa bodaboda ambazo zitatumiwa kuendeshea uhalifu.

Inasikitisha kuwa kati ya bodaboda 1.4 milioni zinazohudumu nchini karibu 100,000 hazijasaliwa rasmi, kulingana na mwenyekiti wa kampuni ya pikipiki ya Honda Motorcyles Kenya Ltd Isaac Kalua.

Wale ambao hawajasajili bodaboda zao watumie utulivu uliopo, baada ya polisi kusitisha msako, kufika katika vituo 52 vya Huduma Centre kote nchini ili kuzisajili.

Huduma hiyo inatolewa bila malipo kwani serikali imefutilia mbali ada ya Sh5,800 iliyokuwa ikitozwa hapo awali.

Wahudumu hao pia waliamriwa kujisajili katika vyama vya akiba na mikopo (Saccos) ambavyo vitahitajika kuwa na sajili ya kidijitali ya wanachama wao ili kutambuliwa kwao.

Kimsingi, serikali irejelee mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti ya jopokazi maalum iliyoteuliwa 2019 kuchunguza changamoto zilizokuwa zikizonga sekta hiyo nyakati hizo, sawa na ilivyo sasa.

Jopokazi hilo liligundua kuwa idadi kubwa ya waendeshaji bodaboda hawajapokea mafunzo uendeshaji katika vyuo vilivyo zilizoidhinishwa na serikali, hawana bima na baadhi yao ni watu umri mdogo wa chini ya miaka 18.

Aidha, sambamba na amri iliyotolewa na Waziri Matiang’i wiki jana jopokazi hilo lilipendekeza kuwa wahudumu wote wasajiliwe katika Saccos na Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF).

Kadhalika wawe wakivalia helmeti na jaketi za usalama nyakati zote wakiwa kazini.Naamini kwamba endapo serikali ingefanikisha utekelezaji wa mapendekezo ya jopokazi hilo, maovu mengi katika sekta hii yangezuiwa.

Visa vya wahudumu wa bodaboda kuwashambulia watu kiholela, kama vile kisa kilichotokea Nairobi juzi havingetokea.

Zachariah Nyaore Obadiah ambaye polisi wanadai ni mshukiwa mkuu katika katika kisa hicho ambapo wahudumu wa bodaboda wanadaiwa kudhulumu kimapenzi mwanamke mmoja afisa wa ubalozi angepatikana haraka zaidi endapo data zake zingekuwa zimehifadhiwa kidijitali.

Kwa hivyo, kwa kuwa serikali imeungama kuwa sekta ya bodaboda huleta mapato ya kima cha Sh365 bilioni kwa mwaka, Hazina ya Kitaifa ikiipata Sh60 bilioni kupitia ushuru wa mafuta, haina budi kuilainisha.

Wahalifu waondolewe katika sekta hii inayowakimu zaidi ya Wakenya 2.4 milioni, wengi wao wakiwa ni vijana waliokamilisha masomo katika viwango mbalimbali lakini hawana ajira.

Wizara ya Usalama, Wizara ya Uchukuzi na ile Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) zishirikiane kuhakikisha kuwa wahudumu hawa wanazingatia sheria za trafiki na kanuni zote zilizowekwa kusimimia sekta hii.

Wajibu huu usiingizwe siasa, haswa wakati kama huu wa kampeni za uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba wanasiasa huwatumia wahudumu hawa wa bodaboda katika shughuli za kuvumisha sera zao mijini na vijijini.

Wanabodaboda watakaovunja sheria waadhibiwe kama watu binafsi huku wenzao wakiachwa kuendelea na biashara zao kama kawaida.