Connect with us

General News

Mapigano ya kikabila yaua zaidi ya watu 70 nchini Sudan Kusini

Published

on

Mapigano ya kikabila yaua zaidi ya watu 70 nchini Sudan Kusini
WATU 72 wameuawa na wengine 11 wamejeruhiwa katika msururu wa mapigano ya kikabila katika mji wa Leer, jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini, kulingana na Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha Kulinda Amani nchini humo (UNMISS).

Kulingana na taarifa iliyotolewa Jumatano jioni, UNMISS pia imenakili visa 64 vya dhuluma za ngono katika eneo hilo.

“UNMISS inalaani vikali ongozeko la visa vya dhuluma za kimapenzi, mauaji kwa kuwakata watu vichwa au kuwateketeza wakiwa hao na mashambulio ya wafanyakazi wa kusambaza misaada ya kibinadamu katika mji wa Leer.

“Hizi ni miongoni mwa vitendo vya ukiukaji wa haki za kibinadamu vilivyotokea wakati wa mapigano yaliyotekelezwa na kundi la vijana wenye silaha, kutoka miji ya Koch na Mayendit kwa kipindi cha wiki moja iliyopita,” kikosi hicho kikasema.

Wanawake wawili walifichua kuwa walibakwa walipotoka katika maficho yao kuwatafutia watoto wao chakula.

“Mwanamke mwingine ambaye juzi alijifungua alielezea kwamba alibakwa na kuchapwa kikatili kwa siku tatu. Nimeshangazwa na mashambulio hayo ya kikatili dhidi ya raia katika mji wa Leer,” akasema mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini Sudan Kusini, Nicholas Haysom.

Alisema kuwa watafanya kila wawezalo kuhakikisha kuwa wahasiriwa na manusura wanapata haki na usaidizi wanayohitaji.

UNMISS inasema kuwa kulingana na ripoti za awali, jumla ya watu 40,000 wamehama makwao kutoroka vita katika mji wa Leer.

Maelfu ya wengine waliripotiwa kuvuka mto Nile na kuingia eneo la Fangak katika jimbo la Jonglei.

UNMISS ilipongeza hatua ambazo serikali imechukua ya kuunda kamati maalum ya kuchunguza vitendo hivyo vya ukiukaji wa haki.

Comments

comments

Facebook

Trending