Connect with us

General News

Maradhi yameangamiza watoto 100,000 – Ripoti – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Maradhi yameangamiza watoto 100,000 – Ripoti – Taifa Leo

Maradhi yameangamiza watoto 100,000 – Ripoti

Na ANGELA OKETCH

KENYA ilipoteza watoto 100,000 wa chini ya umri wa miaka mitano kutokana na maradhi yanayoweza kuepukika mnamo 2020, imebainika.

Homa ya mapafu (nimonia) inaongoza kwa kusababisha idadi kubwa ya vifo vya watoto wa chini ya miaka mitano humu nchini, ikifuatiwa na kushindwa kupumua kati ya maradhi mengineyo.

Ripoti ya Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef), inaonyesha kuwa kati ya waliofariki, 62,000 walikuwa watoto wa kati ya umri wa mwaka mmoja na miaka mitano na waliosalia waliaga dunia kabla ya kufikisha umri wa miezi 12.

“Idadi kubwa ya vifo hivyo vingezuilika,” inasema ripoti hiyo ya Unicef.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa pia linasema kuwa Kenya ilipoteza watu 20,000 wa kati ya umri wa miaka mitano na 14 na watu 14,000 wa kati ya umri wa miaka 14 na 19.

Wakenya 18,000 wa umri wa kubaleghe wa miaka 15 hadi 24 walifariki dunia.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto milioni 5 wa chini ya umri wa miaka mitano walifariki kote duniani mwaka huo.

Vifo hivyo vilirekodiwa katika mataifa 80.

Ripoti inasema kuwa zaidi ya nchi 60, Kenya ikiwemo, hayatatimiza malengo ya kimataifa (SDG) ya kupunguza vifo vya watoto wa chini ya miaka mitano kufikia 2030.

Kulingana na malengo ya SDG, kila nchi inafaa kuhakikisha kuwa inapunguza vifo vya watoto hadi chini ya 12 kwa kila 1,000 wanaozaliwa kufikia 2030.

Nchini Kenya, inakadiriwa kuwa watoto 42 wa chini ya miaka mitano hufariki kwa kila 1,000 wanaozaliwa.

Ripoti hiyo inasema Kenya itashindwa kuafikia malengo ya 2030 kupunguza vifo vya watoto wa chini ya miaka mitano iwapo serikali haitaongeza maradufu juhudi za kulinda afya ya watoto.

Dkt Caroline Mwangi, Mkuu wa Idara ya Watoto na Huduma za Kujifungua katika Wizara ya Afya, alisema idadi hiyo ya juu ya vifo inatokana na huduma mbovu za matibabu kwa watoto wanaozaliwa humu nchini.

Takwimu za wizara ya Afya zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa wakiwa wagonjwa au uzani wa chini ya kilo mbili, hawapewi matibabu yafaayo.

“Idadi ya wauguzi katika hospitali nyingi ni ndogo ikilinganishwa na watoto wanaozaliwa kwa siku,” akasema Dkt Mwangi.

Alisema watu 18 kati ya 1,000 wa kati ya umri wa miaka mitano na 24 walifariki humu nchini mnamo 2020.

Ripoti ya Unicef inasema kuwa asilimia 70 ya vifo vya watu wa kati ya umri wa miaka mitano na 24 vilitokea Barani Afrika (asilimia 45) na Asia (asilimia 26).

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linahimiza mataifa kuongeza juhudi katika utoaji wa chanjo kwa watoto ili kupunguza idadi ya vifo.