Connect with us

General News

Martin Gitonga, Mwalimu wa Kiswahili Mtandaoni – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Martin Gitonga, Mwalimu wa Kiswahili Mtandaoni – Taifa Leo

MWALIMU WA WIKI: Martin Gitonga, Mwalimu wa Kiswahili Mtandaoni

NA CHRIS ADUNGO

MATUMIZI ya vifaa vya kidijitali darasani husisimua wanafunzi, hufanya masomo kuvutia na hukuza ubunifu wa kiteknolojia ndani na nje ya mazingira ya shuleni.

Kuzoesha wanafunzi vyombo mbalimbali vya kiteknolojia kunawafanya wajiamini. Mawanda ya fikira zao hupanuka na maarifa wanayoyachota vitabuni na kutoka kwa walimu wao huchochea hamu ya uvumbuzi ndani yao.

Mwanafunzi akipata umilisi na ujuzi ufaao, atakuwa wa manufaa sana katika jamii ya sasa inayoshuhudia mabadiliko ya kasi kiteknolojia katika takriban nyanja zote.

Haya ni kwa mujibu wa Bw Martin Bin Gitonga ambaye sasa anachapukia ufundishaji wa Kiswahili mitandaoni.

Gitonga almaarufu ‘Malenga wa Bara’ alizaliwa katika kijiji cha Iriga, eneo la Muthambi, Kaunti ya Tharaka Nithi. Ndiye kifungua mimba katika familia ya watoto wawili wa Bw Jasper Gitonga na Bi Harriet Kanyua. Kaka yake ni Boniface Reche.

Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Gituja, Muthambi (1994-2003) kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Muraga, Tharaka Nithi (2004-2007).

Ingawa alisomea shahada ya uanahabari katika taasisi ya mafunzo ya teknolojia ya habari na mawasiliano ya PAGO jijini Nairobi (2008-2010), Gitonga alirejea darasani baada ya miaka mingi ili kutimiza ndoto yake ya ualimu.

“Tamaa ya utangazaji iliyeyuka ghafla nilipopata kibarua cha kufundisha Kiswahili katika shule ya upili ya Wiru, Tharaka Nithi (2012). Nilivutiwa sana na uchambuzi wa Fasihi ya Kiswahili. Awali, nilikuwa nimefundisha katika shule ya upili ya Muraga Girls (2008) kabla ya kujiunga na PAGO,” anasema.

Kwa kuwa alama alizokuwa amejizolea katika KCSE 2007 zilimkosesha nafasi ya kusomea ualimu katika chuo kikuu, alihiari kurudi sekondari baada ya miaka sita na akajiunga na shule ya upili ya Gikurune Boys, Kaunti ya Meru akiwa mwanafunzi wa kidato cha tatu mnamo 2013.

Alifaulu vyema katika KCSE 2014 na akasomea shahada ya ualimu (Kiswahili na Dini) katika Chuo Kikuu cha Kenyatta kuanzia 2015. Baada ya kuhitimu, alifundisha katika shule ya upili ya Katheri Boys, Meru hadi 2021. Aliwahi pia kusomea kozi ya Umilisi wa Taaluma ya Kiswahili katika taasisi ya WASTA, Matasia, Ngong mnamo Oktoba 2010.

Mbali na ualimu, Gitonga ni mfawidhi wa sherehe, mtunzi stadi wa mashairi na mwelekezi wa michezo ya kuigiza. Kipaji chake cha ulumbi kiliwahi kumpa fursa adhimu za kuwa mfawidhi wa mahafali ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (2018), sherehe za kuadhimisha Mashujaa Dei katika Kaunti ya Tharaka Nithi (2020), hafla ya ufunguzi wa Chuo Kikuu cha Chuka Bewa la Chogoria (2019) na sherehe ya ufunguzi wa Chuo cha Kiufundi cha Muraga iliyohudhuriwa na Naibu Rais Dkt William Ruto mnamo Novemba 2019.

Aliwahi pia kuwa mfawidhi wa kampeni za Chama cha Jubilee mnamo 2017 na akawa mratibu wa mawasiliano katika ofisi ya Mbunge Mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti ya Tharaka Nithi, Beatrice Nkatha kati ya 2016 na 2018. Alianza kufundisha Kiswahili mitandaoni baada ya janga la korona kubisha humu nchini mwanzoni mwa 2020.

“Kipindi kirefu cha kufungwa kwa shule kilichochea uvumbuzi mpya. Nilianzisha chaneli ya ‘YouTube’, Kiswahili na Bin Gitonga iliyoziba pengo la ufundishaji wa Kiswahili,” anasema.

Kwa kutumia kipaji chake cha uandishi, amepiga hatua kubwa katika ufundishaji kutokana na upekee wa kuoanisha talanta, ujuzi wa kiteknolojia na taaluma alizozisomea. Maarifa anayojivunia yanamwezesha kupeperusha vipindi mitandaoni kwa wepesi.

Kubwa zaidi katika maazimio yake ni kuwa miongoni mwa walimu watakaobadilisha sura ya ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili kiteknolojia katika enzi hizi za utandawazi.