BI Saada Hamisi, mkazi wa Kichaka Mkwaju, Kaunti ya Kwale, ana wasiwasi kuhusu siku atakayohitaji kujifungua.
Akiwa mmoja wa Wakenya wenye asili ya Kipemba, kabila lisilotambuliwa rasmi na serikali ya Kenya linaloishi katika sehemu za Kaunti za Kwale, Mombasa na Kilifi, hajawahi kupata huduma ya Linda Mama ambayo ni bima ya huduma za afya bila malipo kwa wanawake wajawazito nchini.
“Si mimi pekee niliyeathirika. Wanawake wote Wapemba hupata changamoto wakati wa kujifungua, kwa sababu ni hatari kujifungulia nyumbani na wakienda hospitalini, watatakiwa kulipia huduma,” Bi Hamisi asema.
Anaeleza kuwa wengi wa waume wao ni wavuvi, na wanachopata hakitoshi kuwalisha, mbali na kulipa bili za hospitali kama za baada ya kujifungua.
Yeye ni miongoni mwa watu 7,000 kutoka jamii ya Wapemba wanaoishi Kenya, ambao kwa miongo mingi wameishi nchini bila hati yoyote kuthibitisha kuwa wao ni raia wa Kenya.
Hii imewakosesha huduma muhimu za serikali kwa kutokuwa na vitambulisho.
Mbali na kukosa bima ya afya, Bi Hamisi, anayefanya biashara ndogondogo pia angetamani kujiunga na vyama vya wanawake, lakini hii pia ni ngumu kwake kwani mtu huhitajika kujiandikisha kwa kutumia kitambulisho cha taifa, ambacho hana.
“Siwezi kujiunga na wanawake wengine kwa sababu sina kitambulisho. Wakati mwingine hali inapokuwa mbaya, ninalazimika kuomba mwenzangu atumie kitambuslisho chake ili kunisaidia nijiunge na chama,” akaeleza.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wapemba nchini Kenya, Bw Shaane Hamisi Makame, ambaye ni mvuvi alisema mara nyingi wamekuwa wakikamatwa na polisi wakipatikana wakivua samaki kwa kuwa hawana njia yoyote ya kuthibitisha kuwa wao ni Wakenya walio na haki ya kufanya uvuvi katika bahari za nchi.
Uvuvi na kilimo ndio kitega uchumi kikuu katika jamii ya Wakenya wenye asili ya Kipemba.
“Hatuna chochote cha kuthibitisha uraia wetu. Kwa hivyo, mara nyingi tunapokwenda kuvua tunakamatwa kwa sababu polisi wanafikiria sisi ni Watanzania tunavua samaki kwenye maji ya Kenya kinyume na sheria,” Bw Makame afafanua.
Alisema baadhi ya jamaa zake wameamua kujipatia vitambulisho kwa njia haramu.
Katibu wa jamii hiyo, Bw Ali Mkasha, alisema mbali na kukosa huduma, bado hawatapiga kura katika uchaguzi wa mwaka huu 2022.
Alimuomba Rais Uhuru Kenyatta kuharakisha shughuli hiyo ya kuwatambua kama raia wa Kenya.
Wiki iliyopita, jamii hiyo ilikusanyika eneo la Lungalunga na kuandamana na Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KHRC) kwa matumaini ya kupata majibu kutoka kwa wabunge wanaowawakilisha bungeni.
Walikuwa wameeleza masaibu yao mwaka uliopita kwa Kamati ya Bunge la Kitaifa inyaohusika na Utawala na Usalama iliyozuru maeneo ya Kilifi na Shimoni.
Baada ya hapo, mada hiyo iliyowasilishwa bungeni na Mbunge wa Kilifi Kaskazini, Bw Owen Baya, ilipitishwa na wabunge mwaka jana wakiomba serikali kuwapa Wapemba vitambulisho. Lakini bado jambo hilo halijashughilikiwa.
Bw Baya alisema kuwa bunge hilo tayari limepitisha matakwa yao na anasubiri wizara ya Usalama inayoongozwa na Dakta Fred Matiang’i, kuanza mchakato wa kuwasaidia.
“Tayari tumefanya jukumu letu, aliyebaki ni Rais Uhuru Kenyatta na mahakama ya Wizara ya Mambo ya Ndani na Usalama kufanya uamuzi iwapo atapeana vitambulisho,” Bw Baya aliambia jamii.
Aliongeza kuwa ikiwa Mswada wa Sheria ya Huduma unaotarajiwa kuwasilishwa bungeni hivi karibuni utapitishwa, mambo yatakuwa magumu zaidi kwa Wapemba, na jamii nyingine yoyote isiyo na utaifa nchini.
Hii ni kwa sababu wanachama hawataweza kupokea huduma zozote za serikali kwa kukosa nambari na kadi ya Huduma.
“Pia itamaanisha kuwa hawawezi kwenda hospitalini au hata kuripoti uhalifu kwa kwa sababu ya kutokuwa na thibitisho la uraia,” alisema.
Mbunge wa Lungalunga Khatib Mwashetani naye alisema kuwa ofisi yake imeshindwa kutoa huduma kama vile basari wa kwa kazi wengi kwa sababu wanakosa vitambulisho.
Bw Mwashetani alieleza kuwa watawasilisha barua kwa Dkt Fred Matiang’i kuuliza kwa nini serikali imekwawiaa kuwapa jamii hiyo vitambulisho hata baada ya bunge kuthibitisha kuwa Wapemba ni raia Wakenya.
Wakati huo huo, mashirika mbalimbali ya kutetea haki za kibinadamu zimeahidi kuwa ikiwa serikali itachelewa kuwapa vitambulisho jamii ya Wapemba, watatembea kinyumenyume hadi Ikulu ya Rais Uhuru Kenyatta mjini Nairobi.
“Jambo lolote paka lisukumwe. Tuliamua kutembea na wenzetu wenye jamii ya Wamakonde, na hivi sasa hatua imefika kwamba bunge limekubali kuwa Wapemba wapatiwe vitambulisho, lakini mpaka sasa bado hatujaona ikitekelezwa,” Bw Juma Baro, mmoja wa maafisa wa kutetea haki za kibinadamu alisema.
“Tunatoa wito kwa serikali, la sivyo tutatembea kwa miguu kinyume nyume impaka Nairobi ili watueleze kwa wamechelewa kutekeleza jambo hilo,” Bw Baro alisema.
Jamii nyingine isiyo na uraia katika kaunti ya Kwale ni ile ya Warundi, ambao mwezi jana pia walitoa ombi lao kwa Rais Uhuru Kenyatta kuwapa vitambulisho kabla muhula wao kuisha.