Maseneta walalamikia kuzimwa kuenda mataifa ya kigeni
Na CHARLES WASONGA
MASENETA wa mrengo wa Tangatanga wamelalamikia kile walichokitaja kama hatua ya serikali kuwazuia baadhi ya maseneta kusafiri nje kabla ya kujadiliwa na kupigiwa kura kwa mswada tata wa marekebisho ya sheria ya vyama kisiasa.
Wakiongozwa na Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen, maseneta hao Jumanne, Januari 25, 2022, walisema hatua hiyo ni kinyume cha Katiba na sheria husika.
“Vile vile, hii ni sawa na kuingilia shughuli za seneti ambayo ni asasi huru. Mbona maseneta wazuiwe kwenda nje kwa shughuli rasmi za bunge hili?” akauliza Bw Murkomen ambaye zamani alihudumu kama kiongozi wa wengi.
Alielekeza kidole cha lawama kwa Rais Uhuru Kenyatta akisema ndiye aliyetoa amri hiyo.
Naye Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot alimtaka Spika wa Seneti kuchunguza madai hayo akitaja hatua ya kuzuiwa kwa maseneta kusafiri kuwa sawa na “kuingilia mamlaka ya Spika wa Seneti.”
“Nimepokea habari kwamba maseneta wanaoendelea na shughuli zao zinazohusisha kusafiri nje ya nchi wamezuiliwa kuondoka nchini. Kuna agizo kutoka kwa serikali kuu kwamba hakuna anayepaswa kusafiri nje kabla hatujamaliza kushughulikia mswada wa vyama vya kisiasa. Mheshimiwa Spika, unafaa kuingilia suala hili,” Bw Cheruiyot akaongeza.
Kwa upande wake, Seneta Moses Wetang’ula aliisuta serikali kwa “kulazimisha seneti kupitisha mswada huo.”
“Hakuna sheria inayomlazimu seneta kuketi ukumbini. Na wakati kama huu ambapo tunaweza kushiriki shughuli za bunge hili kupitia mtandao wa Zoom na mbinu nyingine za kiteknolojia, seneta anaweza kushiriki akiwa Amerika na hata Uarabuni,” akasema.
Bw Wetang’ula ambaye pamoja na kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi mnamo Jumapili walibuni ushirikiano wa kisiasa na Naibu Rais William Ruto, alifichua kuwa ana habari kuwa Seneta wa Kwale Issa Boy Juma alizuiliwa kusafiri nje ya nchi.
“Mwenzetu Issa Boy Juma alifika katika uwanja wa ndege na kuelezwa na maafisa wa idara ya uhamiaji kwamba hawezi kusafiri. Hii sio sawa,” akasema Bw Wetang’ula ambaye pia ni kiongozi wa Ford Kenya.
Seneta wa Mandera Maalim Mohamud pia alidai kuwa maafisa wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) walimwarifu kwamba wamepata agizo la kuwazuia maseneta kusafiri.
Spika Kenneth Lusaka aliamuru kwamba madai hayo yachunguzwe akiahidi kutoa ripoti baada ya majuma mawili.
“Hili ni suala lenye uzito mkubwa zaidi. Kwa hivyo, nimeamuru uchunguzi ufanywe na baadaye ripoti itayarishwe. Nitawasilisha ripoti hiyo baada ya wiki mbili,” akasema.
Kauli yake iliungwa mkono na kiongozi wa wachache James Orengo ambaye aliwashauri maseneta wenzake kusitisha mjadala kuhusu suala hilo.
“Binafsi nimewahi kutolewa kwa ndege nyakati za enzi ya utawala chini ya katiba ya zamani. Ningeomba suala hili lijadiliwe kupitia hoja maalum,” akasema Seneta huyo wa Ugenya.
Kiongozi wa wengi Samuel Poghisio aliwakosoa maseneta wa mrengo wa ‘Tangatanga’ kwa kuingiza jina la Rais Kenyatta katika suala hilo “bila sababu maalum.”