Maskini waongezeka utawala wa UhuRuto
NA PETER MBURU
TAKRIBAN Wakenya milioni 16 wametumbukia katika umaskini wakati wa uongozi wa serikali ya Jubilee, ripoti mpya imefichua.
Ripoti hiyo ya Taasisi ya Utafiti na Uchambuzi wa Sera za Umma (Kippra) inaonyesha kuwa kiwango cha umaskini nchini kimepanda kufikia asilimia 63 ya taifa, kutoka asilimia 38.9 ya taifa mnamo 2014, mwaka mmoja tu baada ya serikali ya UhuRuto kuingia uongozini.
Kulingana na takwimu za Benki ya Dunia kuhusu idadi ya Wakenya, Kenya ilikuwa na watu milioni 46.7 mnamo 2014, ambayo imepanda hadi milioni 53.7 kufikia 2020. Kwa kuzingatia takwimu hizi, hii ni kumaanisha kuwa Wakenya maskini walikuwa milioni 18.16 mnamo 2014.
Vilevile, hii ni kumaanisha kuwa idadi ya Wakenya maskini imepanda kufikia 33.8 milioni (ambayo ni asilimia 63 ya milioni 53.7) ama kusema kuwa Wakenya milioni 15,709,595 zaidi wametumbukia katika umaskini kutoka mwaka 2014.
Ripoti hiyo ya Kippra ambayo ilipima vigezo kama ukosefu wa chakula, huduma za afya na lishe bora (hasa kwa watoto), elimu na kuishi katika hali mbaya kubaini viwango vya umaskini nchini inasema kuwa katika kaunti 15 umaskini umeathiri zaidi ya asilimia 80 ya wakazi.
Ripoti hiyo ya Kippra ambayo ilizinduliwa wiki iliyopita inaorodhesha kaunti za Wajir, Mandera na Turkana kuwa zenye kiwango kikubwa zaidi cha matatizo, huku zaidi ya asilimia 90 ya wakazi wakiishi katika umaskini.
Katika kaunti za Marsabit, West Pokot, Bomet, Busia, Kitui, Samburu, Siaya na Migori, kiwango cha umaskini miongoni mwa wakazi ni kati ya asilimia 80 na 88, na asilimia 40 ya wakazi katika kaunti 42 wanakumbwa na umaskini.
Katika kaunti 36, zaidi ya nusu ya wakazi wamesakamwa na umaskini, ripoti hiyo ikaongeza.
Kuhusu umaskini wa chakula, Kippra inasema kuwa zaidi ya nusu ya wakazi wa kaunti za Busia, Mandera, Marsabit, Samburu, Tana River, Turkana na West Pokot, wanakumbwa na ukosefu wa chakula.
Kitaifa, ripoti hiyo inasema kuwa asilimia 35 ya Wakenya wanakumbwa na ukosefu wa chakula, huku ikizitaka serikali za kaunti kuingilia kati utoaji wa huduma za ulinzi wa kijamii, ambapo serikali kuu imeshindwa kuwafikia Wakenya wote wanaozihitaji.
“Kiwango kikubwa cha familia zimekosa bidhaa na huduma muhimu na hii pamoja na matumizi ya chini ya bajeti za mipango ya ulinzi wa kijamii inalegeza juhudi za kupigana na umaskini. Kaunti zinaweza kuimarisha mipango iliyoko ambayo inaweza kupunguza umaskini moja kwa moja ama kwa njia zingine,” taasisi hiyo ikasema katika ripoti.
Kippra aidha imeshauri serikali za kaunti kuanzisha mipango ya ulinzi wa kijamii kulingana na mahitaji yao, ili kuokoa familia zaidi ambazo zinachungulia umaskini.
Kutolewa kwa ripoti hiyo kunakuja wakati hali ya maisha imezidi kuwa ngumu nchini, huku bei za bidhaa muhimu zikipanda mara kwa mara.
Next article
Mradi wa ufugaji nyuki wasaidia jamii kujikimu