Matibabu kukwama madaktari wakianza mgomo
NA LUCY MKANYIKA
HUDUMA za afya katika Kaunti ya Taita Taveta, zinatarajiwa kutatizika baada ya wahudumu kuanza mgomo baridi.
Wahudumu hao walisema wameanza kwa kusitisha huduma kadhaa za upasuaji na kliniki katika hospitali zote za umma na huduma nyingine zitasitishwa baadaye hadi wakati malalamishi yao yatatatuliwa.
Wiki iliyopita, vyama tofauti vinavyowakilisha madaktari, wauguzi, wataalamu wa dawa, wale wa maabara na wasaidizi wa matibabu, walitoa ilani ya kuanza mgomo.
Imebainika hawajalipwa mishahara ya Januari na Februari licha ya kuwa walisitisha mgomo mwingine uliopangwa mwezi jana baada ya mashauriano na serikali ya kaunti.
Mwakilishi wa Chama cha Wahudumu wa Matibabu na Madaktari wa Meno (KMPDU), Dkt Richard Wangai, alisema uongozi wa kaunti hiyo umeonyesha kutojali kuhusu masaibu yao.
“Tangu tulipotoa ilani ya mgomo siku saba zilizopita, hawajaonyesha kujitolea hata kidogo. Hawajatuita hata kwa mashauriano,” akasema.
Juhudi zetu kutafuta msimamo wa serikali ya kaunti kuhusu suala hilo ziligonga mwamba, kwani katibu wa kaunti, Bw Liverson Mghendi, na Waziri wa Afya katika kaunti, Bw John Mwakima, hawaongea nasi.
Mwenyekiti wa Muungano wa Kitaifa wa Wauguzi (KNUN) tawi la kaunti hiyo, Bw Synnette Ogola, alisema mgomo ambao wameanzisha umenuiwa kushinikiza kaunti kutilia maanani mahitaji ya wafanyakazi wake. Kando na mishahara, wamekuwa pia wakishinikiza kuandikishiwa upya bima ya matibabu na kupandishwa
vyeo, na pia kuboreshewa mazingara ya utendakazi.Mgomo huo umeanza wakati ambapo wahudumu wa afya katika Kaunti ya Mombasa pia wametoa ilani ya kuanza mgomo wiki ijayo kwa kuwa hawajalipwa mishahara tangu Januari.
Hivi majuzi, bunge la kaunti liliruhusu serikali hiyo kukopa Sh484 milioni za kulipa wafanyakazi wa kaunti mishahara.Katika Kaunti ya Kwale, wahudumu wa afya walilemaza huduma za matibabu katika hospitali za umma kwa wiki mbili mwezi uliopita wakilalamikia kutolipwa marupurupu na kupandishwa vyeo.
Next article
Raia 1,000 wa Ukraine wakwama Zanzibar