RIWAYA: Maudhui ya sura ya nane na mtiririko wa vitushi sura ya 9
JUMA lililopita tuliangazia familia mpya ya Mwangeka na alivyoendeleza maudhui ya mapenzi na ndoa.
Leo tunaendelea na uhakiki wa maudhui yafuatayo;
Malezi – Ridhaa anadhihirisha malezi mema anavyomshauri mwanawe, naye Mwangeka na Apondi wanawalea vyema wanao.
Umuhimu wa usalama nchini – Apondi anasisitiza umuhimu wa usalama katika hotuba yake unaowawezesha wanajamii kushiriki katika shughuli za kuzalisha mali inayotimiza mahitaji ya kimsingi (chakula, malazi na makazi). Alihimiza kuwa kila mja ana jukumu la kudumisha amani na usalama kwa kuepuka vitendo vya kihalifu na kuwaangaza wahalifu. Pia polisi na wanajeshi wana jukumu kubwa zaidi la kudumisha usalama na amani kwa sababu wamefunzwa maarifa ya kukabili kadhia za jinai na upelelezi. Aidha, wana ujuzi na njia mwafaka za kutatua migogoro na kupalilia maridhiano. Aliwaonya dhidi ya kutaahari kufika palipotokea mkasa. Aliwahimiza kujitolea mhanga na kujiasa dhidi ya njama za kifisadi na nyendo nyingine hasi.
Haki – polisi wasiwe wepesi wa ufyatuaji ovyo wa risasi unaosababisha vifo vya wananchi wasio na hatia.Mhalifu ana haki ya kufikishwa mahakamani na kushtakiwa kabla ya kupewa adhabu.
SURA YA TISA
Mandhari ni katika uwanja wa ndege. Wahusika ni Dick, Buda, Lemi, Tindi, Sauna, Mwangeka na Umu.
Mtiririko wa vitushi
Dick alikuwa katika uwanja wa ndege akisubiri kusafiri. Anatujuza kuwa alishiriki katika ulanguzi wa dawa za kulevya akiwa na umri wa miaka kumi hadi sasa ana umri wa miaka ishirini. Alisafirisha maelfu ya vifurushi vya dawa za kulevya. Alikuwa mraibu wa dawa hizo kwani wakati mwingine alilazimika kuzimeza kama nyenzo ya kuzisafirisha.
Dick alipelekwa kwa Buda alipoibwa na Sauna (mtindo-mbinu rejeshi). Buda alimfunza namna ya kulangua dawa za kulevya. Alihofia kukataa kwani angesingiziwa wizi. Alirejelea kisa cha rafikiye Lemi aliyechomwa kwa tairi akidhaniwa mwizi. Lemi na dadaye aliyekuwa mwanafunzi chuo kikuu, walienda kusherehekea siku ya kuzaliwa kwa Lemi katika kilabu. Walipokuwa wakirejea nyumbani asubuhi, walikutana na mwanamke mmoja njiani aliyekuwa ameibiwa na akaelekeza kidole walipokuwa Lemi na Tindi. Wapitanjia walidhani kuwa Lemi na dadaye ndio wezi. Wakamshika Lemi na kumchoma huku Tindi akitoroka.
Dick alikumbwa na changamoto si haba katika biashara hii haramu. Hakuwa na utulivu licha ya kupata pesa nyingi katika umri mbichi. Aliponea tundu la sindano kunaswa na maafisa wa forodha mara nyingi na wakati mwingine, walinaswa ikabidi mwajiri wao kuwahonga maafisa hao ili waachiliwe huru.
Dick aliamua kuacha biashara ya kulangua dawa za kulevya na kufungua biashara ya kuuza vifaa vya umeme. Alijiunga pia na chuo cha ufundi na kujifunza Teknolojia na Mawasiliano ya Simu. Alipanua biashara yake na kuuza vifaa vya simu. Sasa anasafiri ng’ambo kwa ajili ya kununua vifaa hivyo. Dick alikuwa akijiandaa kusafiri asubuhi hiyo kama ilivyokuwa desturi yake. Alipokuwa akisubiri ndege alikumbuka maisha yake na familia yake katika Mlima wa Simba.Alishangazwa na hatua ya mamake kuwatelekeza. Alikumbuka maneno ya babake kuwa walimwengu ni hasidi kwa kumsababishia uwele. Anashangaa kuhusu hatima ya ndugu zake; Umu na Mwaliko. Anakumbuka Umu akiahidi kuwatunza kwa hali na mali.
Uchambuzi utaendelezwa juma lijalo
Joyce Nekesa
Kapsabet Boys High School