Maumau wawasilisha kesi kortini wakitaka Ruto atimuliwe kazini
NA RICHARD MUNGUTI
SHUJAA wa vita vya Maumau jana Jumatatu aliwasilisha katika mahakama kuu kesi ya kutaka Naibu Rais Dkt William Samoei Ruto atimuliwe kazini.
Mbali na kumkomoa mamlakani, Bw Michael K Kirungia pia anaiomba mahakama imfukuze Dkt Ruto kutoka kwa makazi rasmi katika mtaa wa kifahari wa Karen.
“Dkt Ruto hatekelezi majukumu yake kama inavyoagizwa katika Katiba ya kumsaidia Rais Uhuru Kenyatta bali amejituma kufanya kazi nyingine anazojipatia mwenyewe,” asema Bw Kirungia katika kesi aliyowasilisha katika mahakama kuu ya Milimani jijini Nairobi.
Mlalamishi huyu anaomba mahakama imzime Dkt Ruto kutumia makazi rasmi ya serikali anamoishi kwa sababu “anaendeleza mambo ya kibinafsi kama vile kuandaa mikutano ya kisiasa na kupokea wajumbe wa heri njema wanaomuunga mkono katika azma yake ya kuwania kiti cha Urais katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.”
Anaomba mahakama ipige marufuku mikutano yote ya kisiasa inayoandaliwa katika makazi hayo rasmi ya Naibu wa Rais kwa vile “hayumo serikalini tena.”
Mzee huyo aliye na umri wa zaidi ya miaka 80 ameongeza kusema Dkt Ruto amekihama chama cha Jubilee na kujiunga na chama kingine cha kisiasa cha United Democratic Alliance (UDA) ambacho hakikumteua wakati wa uchaguzi mkuu wa 2017.
Bw Kirungia anaomba mahakama iamue Dkt Ruto amefanya makosa ya uhalifu kwa kukiuka Kifungu nambari 15 kuhusu kiapo cha afisi.
Bw Kirungia amesema Kifungu nambari 22 (1)(2) cha Katiba kimemruhusu kuwasilisha kesi hiyo dhidi ya Dkt Ruto.
Kwa mujibu wa kifungu hicho, mwananchi yeyote ameruhisiwa kuwasilisha kesi katika mahakama kuu kupata maagizo ya utekelezaji wa sheria ipasavyo na viongozi na asasi mbalimbali za serikali.
Mlalamishi huyo aliyeandamana kortini na wanachama wengine wakongwe wa Maumau amesema katika ushahidi aliowasilisha kortini kwamba Dkt Ruto ‘aliyejiondoa serikalini’ anaendelea kutumia pesa za umma kufadhili harakati za kibinafsi alizojituma mwenyewe.
“Mshtakiwa (Dkt Ruto) anaendelea kutumia vibaya pesa za umma kuendeleza kote nchini kampeni zake za kuwania urais kwa tikiti ya chama cha UDA badala ya kutekeleza majukumu anayopewa na Rais Kenyatta,” asema Bw Kirungia katika mawasilisho yake kortini.
Bw Kirungia anasema kuwa Kifungu nambari 147 (1) cha Katiba kimeeleza kwamba Naibu wa Rais ndiye mdogo wa Rais na kwamba atamsaidia Rais kutekeleza majukumu yake.
“Sasa Dkt Ruto anafanya kazi zake sio za kumsaidia Rais Kenyatta kazi kwa mujibu wa sheria,” asema Dkt Kirungia.
Jaji Christine Meoli aliratibisha kesi hiyo kuwa ya dharura na kuamuru isikilizwe Aprili 28, 2022.
Jaji Meoli alimwamuru Bw Kirungia amkabidhi nakala za kesi hiyo Dkt Ruto ili ajibu madai kwamba “amekaidi sheria na kuacha kutekeleza majukumu yake.”
Bw Kirungia amesema kuwa katika kipindi cha 2013-2017, Dkt Ruto alitekeleza kazi yake kwa mujibu wa sheria lakini miaka minne iliyopita amekaidi kazi zake.