Mawaziri 54 kukutana Nairobi kujadili athari za corona kwa elimu
NA BENSON MATHEKA
MAWAZIRI 54 wa Elimu, ni miongoni mwa watungaji sera wanaotarajiwa kukutana Nairobi kwa kongamano la 21 la Mawaziri wa Elimu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola kujadili hali ya elimu baada ya janga la Covid- 19.
Kongamamo hilo litakalofanyika Nairobi kutoka Aprili 27 hadi Aprili 28, limeandaliwa na Serikali ya Kenya kwa ushirikiano na Afisi ya Jumuiya ya Madola chini ya mada ‘Kuwazia upya Elimu kwa Ubunifu, Ukuaji na Udumishaji baada ya Covid 19’.
Lengo la kongamano hilo ni kujadili masuala muhimu ya elimu yanayopaswa kupatiwa kipaumbele katika mataifa 54 wanachama wa Jumuiya ya Madola kuelekea Ajenda ya Maendeleo ya Kudumu ifikapo 2030.
Kongamano hilo litaleta pamoja mawaziri wa elimu, maafisa wakuu wa serikali, walimu, washirika wa maendeleo, mashirika ya kijamii na watungaji sera kubadilishana ufahamu na mbinu bora katika elimu huku ulimwengu ukiendelea kujijenga upya kufuatia athari hasi za janga la Covid 19.
Washiriki katika kongamano hilo pia watajadili hatua za kuchukua na ubunifu unaoweza kutumiwa na nchi wanachama kuweka mifumo ya kudumu na stahimilivu ya elimu.
Kulingana na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Patricia Scotland QC, janga la Covid 19 liliathiri mifumo ya elimu kote ulimwenguni.
“Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, tumeona Covid 19 ikipokonya watu wapendwa wao, kazi zao, shughuli na starehe zao kote ulimwenguni. Athari zake kwa watoto na vijana zimekuwa nyingi huku mamilioni ya wanafunzi wakishuhudia masomo yao yakivurugwa, shule na vyuo vikuu vikifungwa, na wanafunzi kulazimika kusoma wakiwa nyumbani,” alisema Scotland.
Alisema janga hilo pia lilizidisha ukosefu wa usawa hasa kati ya wasichana na jamii zilizotengwa.
Katibu Mkuu huyo alisema kwamba wakati umefika kwa kuzuia janga hilo kupokonya binadamu haki ya elimu.
“Mada ya kongamano hilo linatukumbusha kwamba huu ndio wakati muhimu wa jamii yetu ya Jumuiya ya Madola kuungana kutathmini hali na kujenga Jumuiya yenye ustawi zaidi kwa watoto wetu,” alisema.
Waziri wa Elimu wa Kenya Profesa George Magoha, alisema kwamba COVID-19 ililemaza mifumo ya elimu kote nchini huku nchi za mapato ya chini zikiathiriwa zaidi.
“Huku maisha ya watoto na vijana wetu yakiwa hatarini, tunafa kutia bidii kujijenga tena na kuwekeza katika elimu bora kwa usawa,” alisema.