Mawaziri, makatibu wajiuzulu kujaribu bahati katika siasa
NA LEONARD ONYANGO
MAWAZIRI watatu ni miongoni mwa watumishi wa umma waliojiuzulu kufikia jana ili ku – wania viti mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.
Waziri wa Ugatuzi Charles Keter alipokelewa rasmi na Naibu wa Rais William Ruto katika chama cha United Democratic Alliance (UDA) muda mfupi baada ya kutangaza kujiuzulu jana.
Bw Keter aliyeteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2015 kujiunga na Baraza la Mawaziri, sasa atamenyana na Seneta Aaron Cheruiyot ambaye pia ni mwandani wa Dkt Ruto.
“Nawashukuru maafisa katika wizara za Kawi na Ugatuzi ambapo nilihudumu nikiwa waziri kwa kazi nzuri na ushirikiano mwema,” alisema Bw Keter jana alipotangaza kung’atuka.
Waziri wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Adan Mohamed alijiuzulu huku akisema kuwa amechukua hatua hiyo ili kujiandaa kuwania ugavana wa Mandera katika Uchaguzi Mkuu ujao.
“Tunapokaribia Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2022, nimeamua kwenda kuwatumikia wakazi wa Mandera kama gavana wao. Kwa hivyo, ninajiuzulu kutoka wadhifa wangu wa uwaziri,” akasema Bw Mohamed.
Aliyekuwa waziri wa Madini John Munyes sasa yuko huru kuanza kuendesha kampeni zake za kusaka ugavana wa Kaunti ya Turkana baada ya kujiuzulu jana.
Watumishi wa umma wanaotaka kuwania viti katika uchaguzi ujao wana hadi leo saa sita usiku kujiuzulu kutoka kwa nyadhifa zao.
Kulingana na sheria, watumishi wa umma wanahitaji kujiuzulu kutoka serikalini miezi sita kabla ya Uchaguzi Mkuu.
Katibu wa Wizara ya Maji, Joseph Irungu pia alijiuzulu jana kwenda kuwania ugavana wa Murang’a. Bw Irungu atamenyana na Seneta Irungu Kang’ata aliyezindua kampeni zake rasmi wikendi iliyopita.
Wengine wanaomezea mate kiti hicho ni aliyekuwa mbunge wa Kigumo Jamleck Kamau, mfanyabiashara Stanley Kamau na Moses Mwangi.
Katibu wa Wizara ya Wanyamapori Fred Segor na Mawaziri Wasaidizi (CAS) John Mosonik (Madini) na Joseph Boinnet (Madini) pia walipokelewa rasmi jana ndani ya chama cha UDA.
Bw Boinnet anamezea mate kiti cha ugavana wa Elgeyo Marakwet huku Bw Mosonik akisaka ugavana wa Bomet.
Next article
Wakenya wapewa muda zaidi kujiandikisha katika ofisi za IEBC