Mawaziri wapigia Raila debe uchaguzi ukinukia
CHARLES WASONGA NA BENSON MATHEKA
MAWAZIRI wa Serikali waliosalia baada ya wenzao kujiuzulu kuingia siasa sasa wameanzisha kampeni kali kuvumisha Azimio la Umoja chini ya kinara wa ODM, Raila Odinga.
Mawaziri Peter Munya, (Kilimo) Fred Matiang’i (Usalama), Mutahi Kagwe (Afya), Joe Mucheru (ICT), James Macharia (Uchukuzi), Keriako Tobiko (Mazingira) na Ukur Yatani (Fedha) na Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa sasa wameanzisha kampeni kali kumpigia debe Bw Odinga.
Baadhi ya mbinu wanazotumia ni ziara za kuzindua na kukagua miradi mbalimbali chini ya wizara zao kama majukwaa ya kumpigia debe kiongozi huyo wa ODM.
Hii ni kwa sababu mkubwa wao, Rais Uhuru Kenyatta, amekariri mara si moja kwamba, anamuunga mkono Waziri huyo Mkuu wa zamani kuwa mrithi wake atakapoondoka mamlakani baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, mwaka huu.
Wao hufanya hivyo kwa kutumia rasilimali za serikali, jambo ambalo limeibua maswali miongoni mwa Wakenya na wadadisi wa masuala ya utawala na siasa.
Bw Munya, baada ya kujiondoa kutoka kinyang’anyiro cha ugavana wa Meru, sasa anatumia mikutano ya wakulima kumpigia debe Bw Odinga.
Katika ziara yake ya siku mbili katika kaunti ya Meru, iliyoanza Ijumaa wiki jana, Waziri huyo wa Kilimo aliwataka wakulima na wananchi kuunga mkono Azimio la Umoja kwa sababu “ndio utalinda maslahi yetu”. “Bw Odinga ndiye ana uwezo na moyo wa kutekeleza ajenda za maendeleo
ambazo Rais Kenyatta ameanzisha na huenda hazitakamilika kabla ya kuondoka kwake afisini,” Bw Munya akasema kati – ka soko la Kangeta ambako alikagua ujenzi wa kiwanda cha maziwa cha Nyambene New KCC.
Waziri huyo ambaye anahusishwa na chama cha PNU, alisisitiza kuwa, eneo la Mlima Kenya halialikwi kujiunga na ODM bali ni washirika katika muungano wa Azimio la Umoja pamoja na vyama vyao, akisema hatua hiyo inaashiria heshima.
Naye Waziri Kagwe alitumia shughuli rasmi aliyoongoza mjini Chogoria kama jukwaa la kumpigia debe Bw Odinga huku akiwaonya vijana dhidi ya kumpigia kura “mtu asiyefaa katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.”
“Tayari tumemtambua mtu ambaye ataendeleza mipango na miradi ya serikali inayoendelezwa. Na tunamjua yule ambaye hawezi kufanya hivyo,” akasema.
“Tayari Rais ametuambia Bw Raila ndiye anaweza kuendeleza miradi inayotekelezwa na serikali wakati huu,” Bw Kagwe akaongeza.
Alisema hayo alipozindua rasmi bweni katika Chuo cha Mafunzo ya Kimatibabu cha Clive Irvine katika Hospitali ya Kimesheni cha Chogoria.
Bw Kagwe alisema aliamua kutojiuzulu, ili kuwania nyadhifa za kisiasa, kwa sababu analenga kufanikisha miradi mingi ambayo ingali inaendelea katika wizara yake.
Tangu mwaka jana, Bw Tobiko amekuwa akitumia shughuli rasmi za Wizara yake kama vile upanzi wa miti kumfanyia kampeni Bw Odinga huku akimshambulia na kumdunisha Dkt Ruto.
Mnamo Februari 2, Waziri huyo wa Mazingira alitumia magari na rasilimali zingine za serikali alipohudhuria mkutano wa Azimio la Umoja katika kaunti ya Kajiado.
“Swali kuu ni hili, tuko salama mikononi mwa nani?. Tumpigie kura Raila na tumpeleke Ruto nyumbani kwake Sugoi,” Bw Tobiko akasema.
Mawaziri Wamalwa na Matiang’i wametetea hatua yao ya kumpigia debe Bw Odinga wakisema wanafanya hivyo kwa misingi ya handisheki kati yake na bosi wao, Rais Kenyatta.
“Sihitaji ruhusa ya yeyote kuunga Raila. Wakenya wengi wako mahali Rais na Raila wako na hapo ndipo nilipo” Bw Matiang’i alinukuliwa akisema akiwa Kisii mwaka jana. Bw Wamalwa amekuwa akihudhuria na kuongoza mikutano ya chama cha Democratic Alliance Party of Kenya ambacho kinaunga Azimio la Umoja la Bw Odinga.
“Sisi tuko ndani ya Azimio la Umoja kuunganisha Wakenya wote,” alisema kwenye mkutano Trans Nzoia.
Akieleza sababu za kukataa kujiuzulu kugombea kiti cha ugavana kaunti ya Marsabit alivyokuwa ametangaza awali Waziri wa Fedha Ukur Yatani alisema “nawatakia watu wa Marsabit waongozwe na Mungu kuchagua viongozi wajao kutoka Azimio la Umoja linaloongozwa na Raila Odinga.”
Naye waziri wa uchukuzi James Macharia aliyehudhuria mikutano kadhaa ya Azimio la Umoja jijini Nairobi na Murang’a alisema wazi haoni haya kumpigia debe Bw Odinga.
“Tunasema haya hadharani kwa sababu hatufichi chochote, tutampigia debe Bw Odinga katika miezi sita ijayo,” alisema.
Naye waziri wa ICT, habari na mawasiliano Joe Mucheru amekuwa akiongoza kampeni kali ya kumtangaza Bw Odinga kama rais wa tano wa Kenya
Next article
Seneti kuhoji Yatani kuhusu kuchelewa kwa pesa za kaunti