[ad_1]
Mboma apiku Kipchoge, Kipyegon na kutawazwa Mchezaji Bora wa BBC kutoka Afrika Mwaka wa 2021
Na MASHIRIKA
MTIMKAJI matata raia wa Namibia, Christine Mboma ametawazwa Mchezaji Bora wa Afrika wa Mwaka wa 2021 kwenye tuzo za BBC African Sports Personality of the Year, na kuwa mwanamke wa kwanza katika historia kuwahi kutwaa tuzo hiyo ya haiba.
Mboma, 18, aliweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kutoka Namibia kuwahi kushinda medali ya Olimpiki alipojizolea nishani ya fedha katika mbio za 200m jijini Tokyo, Japan mnamo 2021.
Mboma aliwapiku wanariadha mahiri kutoka Kenya, Eliud Kipchoge na Faith Kipyegon, Ntando Mahlangu anayeshiriki mbio za walemavu nchini Afrika Kusini, kipa wa Senegal Edouard Mendy na muogeleaji wa Afrika Kusini, Tatjana Schoenmaker.
Sasa anakuwa mchezaji wa pili wa Namibia kuwahi kujizolea tuzo hiyo ya haiba kubwa barani Afrika baada ya mtimkaji Frankie Fredericks aliyeshinda taji hilo mnamo 1993 wakati likiitwa BBC African Sports Star of the Year.
Tuzo hiyo baadaye ilianza kuitwa BBC African Footballer of the Year kuanzia 2001 hadi 2018 ambapo wadhamini, Shirika la Habari la BBC, waliliita BBC African Sports Personality of the Year kwa ajili ya kutambua wanamichezo wanaotia fora katika fani nyinginezo mbali na soka.
Mbali na nishani ya fedha katika Olimpiki, Mboma pia alitamalaki mbio za Diamond League na akatwaa dhahabu kwenye Riadha za Dunia za Chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 jijini Nairobi. Alivunja rekodi katika mbio za 200m miongoni mwa chipukizi wa U-20 mara kadhaa mnamo 2021.
Alianza kutamba katika mbio hizo za 200m baada ya kuzuiliwa kushiriki fani aliyoizoea zaidi ya 400m vipimo vilipobainisha kwamba alikuwa na kiwango cha juu cha homoni za testosterone.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO
[ad_2]
Source link