Mbowe aachiliwa baada ya kuzuiliwa seli miezi 8
DAR ES SALAAM, TANZANIA
NA MWANANCHI
KIONGOZI wa Upinzani nchini Tanzania na mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, ameachiliwa huru baada ya kuzuiliwa kwa miezi minane kwa madai ya kuhusika na ugaidi.
Mbowe pamoja na wenzake watatu – Halfani Hassan, Adam Kasekwa na Mohamed Ling’wenya – walifutiliwa mashtaka yote yaliyokuwa yakiwakabili katika mahakama ya rushwa na uhujumu uchumi.
Hassan, Kasekwa na Ling’wenya walikuwa askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika kikosi cha makomando kilichopo Sangasanga, mkoani Morogoro ambao waliachishwa kazi kutokana na sababu za kinidhamu.
Wanne hao walikaniliwa na mashtaka ya kupanga njama kutekeleza vitendo vya kigaidi, kufadhili vitendo vya kigaidi, kushiriki vikao vya kutenda vitendo vya kigaidi na kupatikana
na silaha za kutekelezea vitendo vya ugaidi waliyodaiwa kutenda nyakati na mahali tofauti kati ya Mei 1, 2020 na Agosti 5, 2020 katika mikoa ya Morogoro, Kilimanjaro na Dar es Salaam.
Mbowe aliachiliwa huru wiki mbili baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kukutana nchini Ubelgiji na naibu mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu ambaye alimsihi kuagiza Mbowe aachiliwe bila masharti.
Jumatano, Rais Suluhu alikutana na viongozi wa makanisa katika Ikulu ya Dar es Salaam ambao walimtaka kuachilia huru Mbowe na wenzake bila msharti.
“Viongozi wa kidini walitumia mkutano wao na Rais Suluhu kuomba Mbowe aachiliwe huru,” ilisema taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Ikulu Zuhura Yunus baada ya mkutano huo.
Lissu alikimbilia uhamishoni nchini Ubelgiji baada ya uchaguzi wa 2020
akidai kuwa maisha yake yalikuwa hatarini.
Wanne hao waliachiliwa baada ya mwendesha mashtaka mkuu wa serikali, kuwasilisha ombi la kusema kuwa hakutaka kuendelea na kesi hiyo.
“Taarifa hii tunaiwasilisha kwa njia ya maandishi, kwa maombi hayo ya Kifungu cha 91(1) tunaomba kuondoa mashtaka yote dhidi ya washitakiwa wote,” alisema wakili wa serikali mbele ya jaji Joachim Tiganga ambaye amekua akisimamia kesi hiyo.
Mbowe alitiwa mbaroni jijini Mwanza usiku wa kuamkia Julai 21, 2021 katika mkutano wa kupanga mikakati ya kushinikiza serikali kuandika katiba mpya.
Taarifa ya msemaji wa polisi, David Misime, ilidai kuwa Mbowe hakukamatwa kwa tuhuma za kupanga na kuandaa kongamano la Katiba mpya jijini Mwanza bali alikuwa akiandamwa na kesi ya ugaidi.
Upinzani ulishikilia kuwa kukamatwa kwa Mbowe ilikuwa mbinu ya serikali ya kuzima wapinzani.
Upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi 13 ambao walikamilisha kutoa ushahidi wao dhidi ya Mbowe na wenzake Februari 13, mwaka huu.
Alipokutana na viongozi wa kisiasa Disemba mwaka uliopita, Rais Suluhu alidokeza kuwa yuko tayari kusamehe.
Upinzani umekuwa ukipigania katiba mpya huku ukisema kuwa katiba ya sasa imempa rais mamlaka mengi kupinduki
Next article
DOUGLAS MUTUA: Ubaguzi wa rangi ungalipo na Mwafrika ndiye…