Connect with us

General News

Mbunge adai kuna njama ya kuuza bandari ya Mombasa – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Mbunge adai kuna njama ya kuuza bandari ya Mombasa – Taifa Leo

Mbunge adai kuna njama ya kuuza bandari ya Mombasa

Na BRIAN OCHARO

MBUNGE wa Kilifi Kaskasini, Bw Owen Baya, ameibua upya madai kwamba kuna njama ya kubinafsisha Bandari ya Mombasa.

Mbunge huyo amedai kuwa njama hiyo fiche imelenga kunufaisha watu wachache na kuzidi kuhangaisha wakazi wa Pwani kwa ukosefu wa ajira.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara Mombasa ambao uliongozwa na Naibu Rais William Ruto, Bw Baya alidai kuwa njama hiyo inahusisha kusababisha hasara kwa bandari ili iuzwe kwa bei ya kutupa kwa mwekezaji wa kibinafsi.

“Kuna nia ya kufanya ionekane kwamba bandari imefilisika ili wapate nafasi ya kuibinafsisha. Wanataka kuibinafsisha ndio wachukue pesa zote wapeleke Nairobi ili kuwakosesha watu wetu mishahara,” akasema.

Mbunge huyo ameomba Wapwani hasaa viongozi wasimame kidete ili waweze kuitetea bandari hiyo.

Madai kuhusu ubinafsishaji wa bandari ya Mombasa imekuwepo kwa miaka mingi, ila serikali hukana kuwepo kwa mipango aina hiyo.

Wadau mbalimbali walianza kuibua tena wasiwasi kuhusu mipango hiyo kufuatia ufichuzi kuwa sehemu za bandari zinasimamiwa na mashirika ya kibinafsi kwa njia ambazo zinatiliwa shaka.

Mwezi uliopita, kamati ya bunge inayosimamia masuala ya uwekezaji wa umma ilitaka Mamlaka ya Bandari za Kenya (KPA) kueleza wazi jinsi zabuni za kusimamia sehemu za bandari zilitolewa kwa mashirika ambayo yanahusishwa na wanasiasa na wafanyabiashara mashuhuri.

Wanasiasa wengine ambao walihudhuria mkutano huo wa Dkt Ruto ni wabunge Aisha Jumwa (Malindi), Khatib Mwashetani (Lungalunga), Mohamed Ali (Nyali) miongoni mwa wengine.

Dkt Ruto alikwepa kuzungumzia suala hilo, na badala yake akatetea ujenzi wa reli ya SGR akisema haukusudiwa kuua uchumi wa Pwani.

Reli hiyo ni miongoni mwa sababu ambazo viongozi wa Pwani husema zimechangia kuathiri vibaya uchumi wa Pwani.

Dkt Ruto alidai kuwa, watu wachache waliteka nyara mradi huo kwa maslahi yao ya kibinafsi.

“Tutaweka mpango sahihi wa kufufua uchumi wa eneo hilo. Tunataka kurudisha uchumi wa Mombasa ulipokuwa hapo awali. Lakini lazima tushirikiane ili kutimiza ndoto hii,” akasema.

Baadaye msafara wake ulielekea katika Kaunti ya Kilifi, ambapo wandani wake walimkejeli Gavana wa kaunti hiyo, Bw Amason Kingi kwa tangazo lake kuwa Chama cha Pamoja African Alliance (PAA) kitashirikiana na ODM.

“Wale wanakuja kutuhadaa na vyama vya jikoni twawaambia hatuna wakati,” akasema Bi Jumwa.