MCHEZAJI wa zamani wa Gor Mahia FC Abdulkarim Maqbul amejiunga na Heegan FC inayoshiriki Ligi Kuu nchini Somali kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Akizungumza na Taifa Leo kutoka nchini Somali siku ya Jumatano, Maqbul ameelezea furaha yake kujiunga na timu hiyo iliyo kati ya timu kubwa nchini humo. “ Nimefurahi kujiunga na Heegan mojawapo ya timu kubwa na yenye sifa kuu nchini Somali kwa mkataba wa mwaka mmoja,” akasema mlinzi huyu machachari.
Lakini mlinzi huyu alidinda kufichua kiasi atakachokua akitia kibindoni kila mwezi ila amekiri kuwa ni kiasi kizuri cha kuweza kubadilisha maisha yake. Maqbul alijiunga na K’Ogalo mwaka wa 2017 chini ya kocha Mbrazil Ze Maria akitokea Jericho All Stars na kuwa katika kikosi kilichonyanyua ligi kuu msimu wa 2017/18.
Mashabiki wengi wa K’Ogalo walimpigia upatu kurithi mikoba ya difenda wa kupanda na kushuka Erick ‘ Marcelo ‘ Ouma aliyeekea ughaibuni kujiung na FK Tirana ya Albania. Kuondoka ghafla kwa kocha Ze Maria katika kikosi cha K’Ogalo kulichakachua mipango ya Maqbul na kuamua kurudi timu yake ya zamani ya Jericho All Stars.
Aidha, hadi kufikia anajiunga na Heegan, Maqbul alikuwa akiichezea timu ya Congo Boys iliyokuwa ikishiriki Ligi ya Kitaifa Daraja ya Kwanza msimu ulioisha. Maqbul ameifichulia Taifa Leo kwamba ndoto yake ni kuisakatia timu ya taifa Harambee Stars kabla ya kuelekea ughaibuni kupalilia zaidi kipaji chake.
Mchezaji Abdulkarim Maqbul akizuia mpira kwa kichwa wakati wa mazoezi na mabingwa wa zamani wa ligi kuu nchini Gor Mahia katika uwanja wa Camp Toyoyo, Nairobi. Picha/ HISANI
Katika siku za karibuni wachezaji wengi nchini wamekuwa wakielekea nchini Somali kujiunga na timu mbali mbali nchini humo kutokana na mkataba mzuri wanayotoa kwa wachezaji.