Mgogoro wa tiketi Azimio, raha kwa UDA
NA LEONARD ONYANGO
MUUNGANO wa Azimio la Umoja wake kinara wa ODM Raila Odinga unakabiliwa na hatari ya kupoteza vigogo wakuu huku mvutano kuhusu tiketi ukishika kasi.
Baadhi ya wanasiasa wakuu wa ODM na chama cha Jubilee kinachoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta wametishia kugura muungano wa Azimio iwapo watanyimwa tiketi.
Katika Kaunti ya Kajiado, Gavana Joseph Ole Lenku (Jubilee) na gavana wa zamani David Nkedianye (ODM) wameanza kuvutana kuhusiana tiketi ya muungano wa Azimio la Umoja.
Bw Nkedianye alisusia Mkutano wa Wajumbe wa ODM (NDC) wikendi iliyopita kama njia mojawapo ya kushinikiza Bw Odinga na Rais Kenyatta kumpa tiketi ya moja kwa moja ya Azimio la Umoja.
Bw Nkedianye ametishia kugura muungano huo iwapo hautaandaa kura za mchujo baina yake na Gavana Lenku. Naye Bw Lenku pia ameshikilia kuwa hatakubali kufanya mchujo wa pamoja na Bw Nkedianye.
Mbunge wa Kajiado ya Kati Memusi Kanchory wa ODM pia amekataa kushiriki kura za mchujo pamoja na washindani wake wanaomezea mate kiti hicho kupitia chama cha Jubilee.
Iwapo muungano wa Azimio utaidhinisha Bw Nkedianye na Gavana Lenku kuwania ugavana kupitia vyama vya ODM na Jubilee mtawalia katika Uchaguzi Mkuu ujao, watakuwa katika hatari ya kupoteza kiti hicho kwa mwaniaji wa United Democratic Alliance (UDA).
Wanasiasa ambao wametangaza nia ya kuwania ugavana wa Kajiado kupitia UDA ni wabunge Peris Tobiko (Kajiado Mashariki, Katoo Ole Metito (Kajiado Kusini) na aliyekuwa mkuu wa Mamlaka ya Usalama Barabarani (NTSA) Francis Meja.
Mvutano wa tiketi ya Azimio la Umoja pia umechacha katika Nairobi, Mlima Kenya, Kajiado, Narok na Nakuru huku Jubilee ikitaka wenzao wa IEBC kutosimamisha wawaniaji katika maeneo hayo.
Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni anasema kuwa chama cha Jubilee kinataka kuwa na idadi kubwa ya wabunge kukiwezesha kuwa na usemi mkubwa katika Bunge lijalo.
“Chama cha Jubilee hakijasi – mamisha mwaniaji wa urais; tunaunga mkono kinara wa ODM Raila Odinga. Hivyo chama cha ODM kinafaa kutuachia viti katika baadhi ya maeneo ili tufidie,” anasema Bw Kioni.
Mwenyekiti wa ODM John Mbadi anakiri kwamba muungano wa Azimio la Umoja huenda ukajipata pabaya kuhusu ugavi wa tiketi kwa wawaniaji wake watakaoshiriki kura za mchujo.
“Ni kweli muungano wa Azimio la Umoja utakuwa na kibarua kigumu kutoa tiketi kwa wawaniaji wake haswa katika maeneo ya Nairobi, Pwani, Kaskazini Mashariki na Kaunti za Kisii na Nyamira,” anasema Bw Mbadi.
Kulingana na Bw Mbadi, Azimio la Umoja unaendelea kujizolea umaarufu katika maeneo mbalimbali nchini kama vile eneo la Mlima Kenya ambapo wanasiasa wanahama vyama vyao na kuja kutafuta tiketi ya muungano huo.
Katika Kaunti ya Nairobi, viongozi wa ODM wameshikilia kuwa mwaniaji wa ugavana wa chama hicho ni lazima awe debeni katika Agosti 9. Chama cha ODM tayari kimetangaza mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi kuwa mwaniaji wake wa ugavana Nairobi. Upande wa Jubilee unapigia debe mfanyabiashara Richard Ngatia.
Next article
Amerika, NATO hawatamuweza Putin kwa sasa