Mgonjwa afa kwenye safari ya ICU kilomita 520
NA STEPHEN ODUOR
FAMILIA katika Kaunti ya Tana River, imelaumu serikali ya kaunti hiyo kwa kifo cha jamaa wao aliyefariki wakisafiri umbali wa takriban kilomita 520 wakitafuta chumba cha kulaza wagonjwa mahututi.
Familia ya Hussein Hassan, ilikuwa inamsafirisha mzee huyo, 67, kutoka Hola hadi Kaunti ya Meru Ijumaa iliyopita.
“Ndugu yangu alianguka ghafla ndani ya nyumba mwendo wa saa mbili usiku, tukamkimbiza katika Hospitali ya Rufaa ya Hola ambako alifanyiwa upasuaji,” anasimulia Abdi Hassan.
Baada ya upasuaji, madaktari waligundua alihitaji kuwekwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi.
Hospitali ya rufaa ya Hola haina kituo aina hiyo, kwa hivyo walilazimika kumpa mgonjwa rufaa.
“Walipiga simu hospitali zote za mkoa huo wakitafuta nafasi ya ICU, zote zilikuwa zimejaa. Daktari alipiga simu kwa rafiki yake katika Hospi – tali ya Chogoria ambaye alipata nafasi,” alisimulia.
Ilichukua zaidi ya saa sita kwa familia hiyo kupata msaada wa gari la wagonjwa na tanki la oksijeni.
Walisimulia kuwa, safari kwenye barabara mbovu ilileta mashaka mengi, huku mgonjwa akiwa katika hali mbaya, walifaulu kumuombea tu uhai.
Ilikuwa ni safari ya dua kwa kila hatua, huku nduli wa kifo akiwaandama aste aste katika giza hilo totoro hadi walipofika Matuu ambapo tanki la ok – sijeni walilokuwa nalo lilipoisha hewa.
“Tulienda kuomba ambulensi maalum katika Hospitali ya Matuu, wakatusaidia haraka na hata kutupatia dereva ili tuendelee na safari,” alisema Bw Abdi.
Katika Kaunti ya Embu, dakika chache tu kabla ya kufika hospitalini, Hussein Hassan alitumia nguvu kidogo iliyosalia kwake kushika mkono wa nduguye kama ishara ya kumuaga kabla hajafariki.
Muuguzi alithibitisha kifo hicho, dereva alipunguza mwendo wa gari na kusimama, na kwa pamoja wakaomboleza na familia kabla ya kuanza safari ya kurudi nyumbani.
“Tulijisikia vibaya sana. Tunajua kuwa madaktari wa Kaunti walifanya kazi yao vizuri sana, lakini usimamizi wa Kaunti ndio wa kulaumiwa kwa kifo hiki,” jamaa wa marehemu, Bw Harun Hassan alisema.
Kulingana na Harun, gharama walizotumia zingeweza kupunguzwa ikiwa tu utawala wa kaunti hiyo ungetimiza wajibu wake.
Hospitali ya rufaa iliyo na vifaa vinavyofaa ni moja tu ya ahadi ambazo zilitolewa na viongozi waliofuata walipochukua uongozi wa kaunti hiyo.
Kwa takriban miaka 10 sasa tangu mfumo wa ugatuzi uanze, hospitali hizo bado zinakabiliwa na matatizo hayo hayo licha ya kuwa na mabilioni ya shilingi ya hela kutoka katika Hazina ya Kitaifa.
Wiki iliyopita, Gavana wa Tana River, Bw Dhadho Godhana, alikuwa miongoni mwa magavana waliohudhuria hafla ya upanuzi wa mpango wa Afya kwa Wote (UHC) mjini Mombasa, ambao uliongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.
Katika hafla hiyo, Bw Godhana alionekana kukiri kuwa kuna tatizo la kimaendeleo katika kaunti yake huku akitaka serikali ya kitaifa ichangie kuleta mabadiliko.
“Tukikaa na watu wa kaunti nyingine twaambiwa mengi ambayo yamefanyika, lakini kule kwetu ni hafi – fu. Tungependa pia kule Tana kufunguke,” gavana huyo wa pili wa Tana River akamwambia Rais Kenyatta.