Migawanyiko yatokea katika mrengo wa Azimio magharibi mwa Kenya
SHABAN MAKOKHA Na CHARLES WASONGA
MIGAWANYIKO inashuhudiwa ndani ya muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya katika eneo la Magharibi baada ya vyama tanzu kutofautiana kuhusu udhamini wa wagombeaji.
Chama cha ODM chake mgombeaji wa urais wa muugano huo Raila Odinga kinavutana na chama kipya cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) ambacho kimekuwa kikipokea wanasiasa waliohama vyama vya ANC na Ford-Kenya.
Mgongano kati ya ODM na DAP-Kenya unatokea baada ya viongozi wakuu wa vyama hivyo kusisitiza kuwa kila kimoja kitadhamini wagombeaji katika nyadhifa zote isipokuwa ule wa urais.
Naibu Kiongozi wa ODM Wycliffe Oparanya na mlezi – patron – wa DAP-Kenya Eugene Wamalwa huenda wakakabiliana kisiasa na hivyo kuigharimu Azimio la Umoja baada ya kila mmoja kuapa kuwafanyia kampeni wawaniaji wa vyama vyao.
Kwa upande mwingine, Bw Wamalwa ameahidi kuanzisha kampeni ya siku tano katika eneo la magharibi kuvumisha chama chake na wagombeaji wake ili kuyeyusha ushawishi wa ODM ambayo kiongozi wake alifanya ziara ya siku tano eneo hilo wiki jana.
Katika ziara yake Bw Odinga alitoa tiketi za moja kwa moja kwa wabunge; Peter Nabulindo (Matungu), Tindi Mwale (Butere), Christopher Aseka (Khwisero), Titus Khamala (Lurambi), Emmanuel Wangwe (Navakholo) na Bernard Shinali (Ikolomani).
Mbunge wa Teso Kaskazini Oku Kaunya ndiye Mbunge kutoka kaunti ya Busia aliyepata tiketi ya kutetea kiti chake.
Akiongea alipoandamana na Bw Odinga, Bw Oparanya alisema wajibu wake mkuu utakuwa ni kuvumisha ODM katika eneo hilo.
“ODM ndicho chama kongwe na maarufu zaidi katika eneo la Magharibi na nchini. Katika uchaguzi mkuu wa 2017 tuliandikisha matokeo mabaya katika eneo hili na wakati huu hatutaki kupoteza tena. Hii ndio maana tunataka kufanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa ni wagombeaji wa chama chetu watakaochaguliwa,” Bw Oparanya akasema.
Mnamo Alhamisi, wakati wa hafla ya kumtangaza rasmi mgombeaji wa kiti cha ubunge cha Mumias Mashariki kwa tiketi ya DAP-K, Peter Salasya, katika kijiji cha Eluche, Bw Wamalwa alisema chama hicho kinataka kudhibiti siasa za eneo la Magharibi.
Waziri huyo wa Ulinzi alisema walijiunga na vuguvugu la Azimio la Umoja ili kuimarisha nafasi ya Raila Odinga kushinda urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Bw Wamalwa alikana madai kuwa ODM ndicho chama chenye nguvu zaidi katika eneo la magharibi, akisema vyama vyote vya kisiasa ndani ya Azimio la Umoja vina haki sawa.
“Hii ndio maana kama DAP- K, tutadhamini wagombeaji katika viti vyote isipokuwa kiti cha urais, ambacho kimetengewa Bw Raila Odinga. Tutang’ang’ania viti vya ugavana, useneta, ubunge na udiwani,” akaeleza.
Next article
Wakulima wa parachichi watumie vyema fursa iliyoko ya…