Connect with us

General News

Miradi isikwame Rais akistaafu, ajaye aiendeleze – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Miradi isikwame Rais akistaafu, ajaye aiendeleze – Taifa Leo

DOUGLAS MUTUA: Miradi isikwame Rais akistaafu, ajaye aiendeleze

Na DOUGLAS MUTUA

IMEKUWA desturi kwa miradi muhimu nchini kukwama kila wakati serikali inapobadilika na hivyo basi mabilioni ya pesa za walipa ushuru kutumiwa visivyo.

Huu ukiwa mwaka ambapo serikali ya sasa itaipisha nyingine, juhudi zinapaswa kufanywa ili kuhakikisha miradi muhimu iliyoanzishwa haitakwama.

Pesa ambazo hutumika kuanzisha miradi hiyo kisha ikaishia kupuuzwa na kusahaulika ni ithibati ya jinsi ushindani wa matakwa ya kisiasa huiletea nchi hasara.

Mathalan, eneo la Pwani kipo Chuo Cha Utalii Cha Ronald Ngala (RNUC) kilichonuiwa kuwa bora zaidi kwenye kanda hii katika mafunzo ya utalii.

Chuo hicho kilichoanzishwa na Rais Mstaafu Mwai Kibaki kimetokea kutelekezwa na Rais Uhuru Kenyatta, lakini tayari kimetumia Sh4 bilioni na ushei!

Kinahitaji pesa nyingine kama hizo au zaidi, hakijasajili mwanafunzi hata mmoja, na kuna hakika kwamba utawala wa sasa ukiondoka hakitakuwa kimekamilika.

Hakuna hakika utawala utakaokuja utakitilia maanani, hivyo kuna uwezekano kwamba pesa zote hizo ambapo ni ushuru wangu nawe zitapotea hivyo tu.

Je, unaukumbuka ule mji wa kiteknolojia wa Konza City ulioanzishwa na Rais Kibaki yapata miaka 14 iliyopita?

Mpaka sasa haujakamilika, ni jumba moja tu linalokuashiria kuwa hapo pananuiwa kujengwa kitu, na huenda ukakwama zaidi utawala ujao usipotia nia kuukamilisha.

Huo ni mradi uliosifiwa na kutabiriwa kuwa ungekuwa bora na wa kipekee barani Afrika, ambao kwao nafasi za kazi zingebuniwa na mwonekano wa Kenya kubadilishwa kabisa.

Tangu serikali ya Jubilee ichukue hatamu za uongozi, mradi huo umekuwa ukifadhiliwa shingo upande, ujenzi nao ukifanyika iwe yawe tu, wala hakuna anayeonekana kujali.

Imekuwa desturi yetu kuchoma pesa kwa miradi isiyokamilika; serikali moja ikibadilika, inayoirithi haionekani kuwa na nia ya kuzingatia sera zingawa bora namna gani.

Rais Kenyatta alipoingia mamlakani mnamo 2013, aliingia mbioni kukopa mabilioni ya mafedha ili kufanikisha ndoto yake ya kujenga reli na barabara, nyingine tusizohitaji!

Sina haja kurudia kwamba reli aliyojenga kuanzia Pwani hadi Naivasha iliipokonya kazi bandari ya Mombasa iliyokuwa na nafasi bora ya kuifaa nchi.

Akija kiongozi mwingine anuie kubadilisha mambo, hasa kurekebisha hitilafu hiyo ya bandari kujengwa bara hali ufuo wa bahari upo, mabilioni ya pesa yatapotea.

Mkenya, maskini asiye na usemi katika mambo hayo ya ngazi za juu, atabaki kulipa deni la Mchina huku akinufaika kidogo sana kutokana na miradi hiyo.

Ukizuru maeneo mengi nchini, utapata miradi mingi tu ya barabara ikiendelea. Nina hakika hazitakamilika kabla ya Rais Kenyatta kustaafu.

Je, hatima ya barabara hizo ni gani, hasa ikizingatiwa kuwa hakuna sheria inayomwajibisha kiongozi atakayekuja kuikamilisha miradi ya mtangulizi wake?

La hakika ni kwamba zipo pesa zitakazopotea, matingatinga yataachwa barabarani na wanakandarasi hadi itakapokuja serikali nyingine yenye nia ya kujenga barabara. Aibu!

Ninaelewa kila serikali huwa na manifesto ya kuzingatia, sera ambazo ingetaka kutekeleza katika muda wa utawala wake, lakini wote ni ubatili ikiwa mwananchi ataumia.

Nia ya kila serikali inapaswa kuwa kumwondolea mwananchi mateso, kumwokolea pesa na kumtua mzigo mzito wa madeni aliotwikwa na serikali iliyotangulia.

Maisha yanapaswa kuwa bora kutoka utawala mmoja hadi mwingine, lakini nchini Kenya hiyo haiwi nia ya watawala. Lao moja tu: kubuni nafasi za kupora mali ya umma.

Tatizo kuu ni kwamba kila anayeingia ikulu huichukulia fursa hiyo kuwa ya kujitajirisha pamoja na washirika wake wa karibu, sio kututatulia matatizo yetu.

Watawala huwana kwa meno na kucha kuunda pesa za kutosha ili masaibu yanayotusibu sisi kina yakhe yasiwakaribie hata kidogo.

Kenya itakuwa nchi ya kujivunia pale utakapopatikana uhakika wa mwendelezo wa miradi ya serikali moja hadi nyingine. Vinginevyo, tujiandalie mateso.

[email protected]

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Facebook

Trending