Miradi ya kisasa yatia uchungu ‘Lamu tamu’
Na KALUME KAZUNGU
KWA WENGI, MSEMO wa ‘mgeni njoo mwenyeji apone’ huonekana kuwa wa maana kwa vile mgeni hutarajiwa atawasili kwa baraka tele.
Lakini kwa wenyeji wa Lamu, inaonekana ujio wa mgeni kwa jina la ‘maendeleo’ umeanza kuwa laana kwao.Wazee ambao wameishi katika Kaunti ya Lamu tangu utotoni wanasema ijapokuwa maendeleo ni muhimu, wameanza kushuhudia athari mbaya za miradi mikubwa.
Kuanzia sura ya majengo ya kitamaduni hadi tabia zilizozingatia mila na tamaduni za Waamu, mambo yameanza kubadilika kwani maendeleo hayo yamevutia idadi kubwa ya wawekezaji na wakazi kutoka maeneo mengine ya nchi na kimataifa.
Mojawapo ya mabadiliko ambayo yameteka kaunti hiyo ni mbinu za uchukuzi.Miaka iliyopita, wageni wa kimataifa walivutiwa na jinsi kisiwa cha Lamu kilitegemea punda kwa usafiri.Mbinu hiyo ya usafiri ilikuwa ikisifiwa sana na wenyeji kwa kutunza mazingira, kwa vile hapakuwa na uchafuzi wa hewa unaotokana na petroli, kando na kutokuwepo kelele nyingi za magari au hatari ya wapita njia kugongwa barabarani.
Hii leo, zaidi ya wahudumu 400 wa boda boda wanatekeleza shughuli zao ndani ya mji wa Lamu na juhudi za kuwaondoa zimegonga mwamba.Mzee Muhashiam Famau, anasema licha ya pikipiki hizo kutoa nafasi za ajira kwa vijana wengi, mji huo wa kale uliosifika kwa utulivu wake sasa umesheheni kelele za mingurumo ya pikipiki usiku na mchana.
Inahofiwa kuwa, matukio haya yanaweza kufanya Lamu ipokonywe hadhi yake iliyotwikwa mwaka wa 2001, ambapo mji huo uliorodheshwa na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kama sehemu mojawapo ulimwenguni inayotambulika zaidi kwa kuhifadhi tamaduni na ukale wake.
Ongezeko la watu waliovutiwa na nafasi za ajira katika miradi ya serikali pia limechangia kuvuruga utamu wa Lamu.Wafanyabiashara walioona nafasi ya kuwahudumia wananchi wanaoongezeka, waliamua kujenga vibanda kiholela ikiwemo maeneo mkabala na ufuo wa bahari, hivyo kubadili sura asili ya mji.
Ujenzi kiholela
Kulingana na mzee Ghalib Alwy, Serikali ya Kaunti ya Lamu haitakuwa na budi ila kuibuka na mbinu itakayodhibiti ujenzi wa kiholela wa vibanda na hata nyumba. Kando na vibanda hiyo, hitaji la nyumba za kukodishia idadi kubwa ya watu wanaoongezeka Lamu limetajwa kuathiri muundo asili wa eneo hilo.
Inahofiwa kuwa hali isipodhibitiwa, baadhi ya nyumba za kale zilizovutia watalii zitaanza kubomolewa hivi karibuni, kwani hata sehemu za ardhi zilizo na makaburi ya jadi yaliyokuwa yakilindwa sasa zimeanza kumezewa mate na wawekezaji wa kibinafsi.
Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo ulibaini kuwa baadhi ya ramani za nyumba zinazojengwa, hasa kwenye mji wa kihistoria wa Lamu siyo zile zinazokubalika.Ramani za jadi za nyumba zinazokubalika kujengwa katika kisiwa cha Lamu ni zile za asili ya Omani.
Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Lamu, Bw Mohamed Mbwana, anasema haieleweki jinsi ramani za kisasa za nyumba zimeanza kutumiwa ndani ya kisiwa cha Lamu. Katika masuala ya kijamii, Kisiwa cha Lamu ni eneo ambalo idadi kubwa ya wakazi ni Wabajuni waumini wa Kiislamu.
Hii inamaanisha mavazi, hasa kwa wanawake lazima yawe nadhifu.Hata hivyo, wenyeji wanalalamika kuwa katika siku za hivi majuzi, wanawake wengi wamekuwa wakivalia minisketi ambazo huishia kuacha sehemu nyingi za mwili zinazohesabiwa kuwa nyeti kidini zikionekana.
Kwa mujibu wa Mzee Said Seif, Ujenzi wa Bandari ya Lamu (Lapsset) eneo la Kililana umevutia wengi kuja Lamu ili kutafuta ajira.“Wageni, hasa wanawake wanaozuru Lamu au wale wanaofanya kazi katika bandari huvalia mavazi ambayo si nadhifu kwa dini yetu, ikiwemo minisketi.
Wamewafanya baadhi ya wenyeji wa hapa pia kuiga mtindo huo wa mavazi, hivyo kupotoka kabisa kimaadili,” akasema Bw Seif.Athari za kiuchumi pia zimeshuhudiwa kwa wakazi wengi ambao walikuwa wakitegemea riziki kwa uvuvi.
Kulingana na Mwenyekiti wa Muungano wa Lamu Women Alliance, Bi Raya Famau, wavuvi walipoteza sehemu zao za uvuvi walipopisha ujenzi wa bandari ya Lamu. wamekosa mapato, na hali hii imeanza kusababisha mizozo ya kinyumbani.
Ukosefu wa usalama pia umeanza kuibua changamoto, wazee wakisema zamani visa vya wizi mabarazani na vichochoroni hasa kwenye mji wa kale wa Lamu vimeongezeka.
Next article
Kaunti yajitetea kuhusu usafiri uliomeza Sh410m