Misako Makutano
NA MWANGI MUIRURI
[email protected]
MISAKO mikali dhidi ya mitandao ya uhalifu imezinduliwa katika mtaa wa Makutano ulio katika njiapanda za kuelekea katika miji ya Nyeri, Embu na Meru.
Uhalifu huo unajumuisha ukahaba, wizi wa mafuta kutoka magari ya uchukuzi, usambazaji bangi kutoka Kaunti za Kaskazini Mashariki, ulanguzi wa maharamia na uchezaji kamari jinsi ambavyo Taifa Leo ilifichua kwenye makala maalum ya mnamo Machi 15, 2022.
Misako hiyo pia inalenga wezi mtaani na wapakiaji pombe haramu sambamba na wamiliki wa baa ambao hukiuka sheria za biashara ya pombe na mvinyo.
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi wa Mbeere Kusini Bw Gregory Mutiso, hali ya utiifu kwa sheria ndiyo inarejeshwa katika mtaa huo.
“Ningetaka ufike mtaa huo na unionyeshe mtambo mmoja tu wa kucheza kamari. Kwa sasa, wamiliki wa baa watano wamekamatwa kwa kukiuka sheria za kuhudumu huku makahaba wakiwa waneonywa kuhusu uharamu wa harakati zao,” akasema mnamo Machi 25, 2022.
Bw Mutiso aliongeza kuwa doria mtaani zimeimarishwa ili kuwatambua kila aina ya majambazi na amri ni kwamba kusiwe na huruma dhidi ya kila aina ya ukiukaji wa sheria.
Wenyeji tuliowahoji walisema kuwa wameshuhudia mwamko mpya ambapo maafisa wa polisi wa Makutano ambao kwa muda walikuwa wamezembea, sasa wameonekana kutia bidii kazini.
“Mimi nimeshuhudia kahaba mmoja akitiwa mbaroni kwa madai ya kuiba Sh4,500 kutoka kwa mteja wake. Kisa hicho cha Ijumaa asubuhi kimetupa matumaini kwamba maafisa hawa wako tayari kutekeleza sheria,” akasema mmoja wa wenyeji.
Katika kisa hicho cha kahaba kudaiwa kumwibia mteja wake, ripoti iliyoandikishwa katika kituo cha polisi Makutano inaelezea jinsi mwanamume huyo alivyojitokeza na akaingia katika maafikiano ya uteja wa Sh300.
“Nilikuwa nipimiwe mapenzi ya Sh200 huku nikilipa ada ya nyumba ya Sh100. Lakini mwanadada huyo alinigeuka na kinidhulumu nilipompa Sh500 za kugharimia huduma hiyo. Alikataa kunihudumia na akiwa na wengine watano, walinivamia na kunipokonya Sh4,000 nilizokuwa nazo kwa mfuko huku wakinipiga kwa vigongo,” akasema.
Mzee huyo alilalamika rasmi na akapewa barua ya kusaidiwa kupata ukaguzi na matibabu katika hospitali ili kubaini kiwango cha majeraha.
Akirejesha ripoti ya daktari, kahaba huyo pamoja na washirika wake watatiwa mbaroni na kushtakiwa kwa wizi wa mabavu.
Bw Mutiso alisema kuwa serikali imejitolea kuhakikisha kwamba kila mkazi wa Makutano amepata usalama wa kutosha, akiongeza kuwa misako hiyo itasalia hadi hali ya kawaida irejee.
Makutano ni mji mdogo uliojaa vumbi, takataka katika barabara za chorochoroni na maji taka ambayo hujitoa kutoka vioo vya nyumba za makazi na kutapakaa barabarani.
Ni hivi karibuni ambapo kulizuka kilio cha wenyeji ambao walilalamika kuwa kuna jumba moja la biashara ya ngono ambapo watoto wa shule wa kiume na wa kike walikuwa wakionekana wakiingia kushiriki ngono kiholela.
Mji huu hufurika watu kwa kuwa uko katika mpaka wa Kaunti za Embu, Kirinyaga, Machakos na Murang’a na biashara za udalali wa mavuno ya mashambani, mawe ya mijengo, miraa na kila aina ya bidhaa na huduma za ukora huwa imenoga.
Matukio ya ukora huo wote yalikuwa yamenakiliwa kutoka ripoti rasmi za wenyeji zikiwa zimenakiliwa katika vitengo vya wadumisha usalama chini ya jumbe EMB0741237, EMB0741237, EMB5192632, EMB8849793, EMB3245574 na EMB4879251.
Jumbe hizi husambazwa kwa makao makuu ya usalama wa nchi na pia wakuu wote wa kiusalama wa Kaunti hiyo ya Embu.
Afisa wa ngazi ya juu katika Afisi ya Rais (OP) Bw Wilfred Nyagwanga alisema kwamba habari za mtaa huo “zilipokelewa kwa mshangao mkuu na maafisa wa usalama wa eneo hilo wameamrishwa kushughulikia hali hiyo kwa umakinifu unaofaa.”