Mjane ashinda mzozo wa urithi miaka 8 baadaye
NA BRIAN OCHARO
MJANE na watoto wake wawili ambao walikuwa wamefungiwa nje ya urithi wa mali ya mumewe, wameshinda kesi ya kupigania urithi huo mahakamani baada ya zaidi ya miaka minane.
Bi Josephine Wanjiru na watoto wake wawili, walikuwa wamenyimwa urithi kwa madai kuwa ndoa yao haikulindwa kwa msingi wa Sharia za Kiislamu.
Jaribio la mwanamke huyo kupigania haki ya watoto wake lilishindikana mara mbili baada ya ombi lake kukataliwa na Mahakama ya Kadhi na Mahakama ya Kitengo cha Familia huko Mombasa mnamo 2013 na 2015.
Katika uamuzi kuhusu rufaa aliyowasilisha, Jaji John Onyiego alisema watoto hao wawili hawakufaa kuzuiwa kurithi mali ya baba yao kwa kuzingatia swala la kuwa wazazi wao walikuwa wa dini tofauti na kwamba hawakurasimisha ndoa yao inavyotakikana kidini.
‘Kwa kuwa uzazi wa watoto haujapingwa, watoto hawawezi kuadhibiwa kwa kunyimwa kilicho chao kisheria kutokana na kushindwa kwa wazazi wao kuhalalisha ndoa yao,’ alisema Jaji huyo.
Jaji Onyiego aliamuru watoto hao wagawiwe mali kwa mgao sawa.
‘Wasimamizi wa mirathi hawana lingine ila kutekeleza agizo ya kugawa asilimia 9.21 ya hisa wanazostahili kupewa kutoka kwa sehemu ambayo marehemu baba yao alistahili kugawiwa kutoka kwa mali ya babu yao,’ Jaji huyo alisema.
Bi Wanjiru alianza kupigania haki ya watoto wake kurithi mali ya marehemu baba yao kufuatia kifo chake mwaka wa 2012. Alikuwa ameishi na Bw Swauriqy Chuba kama mume na mke kuanzia 1992 hadi alipofariki.
Wakati wa kifo chake, Bw Chuba alikuwa amewasilisha ombi kwa Mahakama ya Kadhi ya Mombasa akitaka mali ya baba yake igawiwe kati yake na mandugu zake kwa mujibu wa Sharia ya Kiislamu kuhusu urithi.
Mahakama ya Kadhi ilitoa uamuzi Agosti 29, 2013 baada ya kifo cha Bw Chuba, kuwa mjane huyo na watoto wake waliozaliwa nje ya ndoa hawakuwa na haki ya kurithi mali hiyo.
Kadhi, hata hivyo, alitambua kuwa mume wa mjane huyo alikuwa na haki ya kupata asilimia 9.21 ya mali ya babake.
Ingawa Bi Wanjiru hakushiriki katika kesi hiyo mbele ya mahakama ya Kadhi, baada ya hukumu kutolewa ndipo alirejea katika mahakama hiyo na kutaka kubatilisha uamuzi wa kuwafungia yeye na watoto wake nje ya hisa za mume wake.
Alidai kuwa uamuzi wa Kadhi Mkuu ulikinzana na Katiba ya Kenya na kwamba alihukumiwa bila kusikilizwa.
Bi Wanjiru pia alilalamika kwamba yeye si Mwislamu hivyo basi haikufaa kesi hiyo ifanyike katika mahakama ya Kadhi.
Lakini ombi lake lilikataliwa baada ya Kadhi Mkuu kushikilia kuwa chini ya Sharia za Kiislamu, yeye na watato wake hawawezi kurithi mali ya marehemu kwa sababu ya kutokuwa Waislamu.
Mwanamke huyo alielekea katika Mahakama Kuu ili kuingilia kati. Hapa, alimwomba Jaji Mugure Thande kubainisha hisa za marehemu mumewe katika shamba kubwa la baba yao na amri ya ziada ya kuzuia wasimamizi wa mali hiyo kugawa au kutenga sehemu hiyo.
‘Mimi si Muislamu kwa hivyo ilikuwa ni makosa kesi hii kusikizwa na kuamuliwa na Mahakama ya Kadhi. Kwa vyovyote vile,” alisema.
Mashemeji zake walipinga ombi hilo na wakamtaka jaji kushikilia msimamo wa Kadhi. Katika uamuzi wake wa Desemba 15, 2015, Jaji Thande alitupilia mbali ombi lake na kuunga mkono maamuzi ya kadhi kwamba yeye na watoto wake hawawezi kurithi mali hiyo.
Mwanamke huyo alikata rufaa katika dhidi yake uamuzi wa jaji Thande.
Mahakama hii ilikubaliana naye kwa kubaini kwamba yeye na watoto wake hawakuwa Waislamu, waliwekwa kimakosa chini ya mamlaka ya Mahakama ya Kadhi.
Next article
EACC yaagiza madiwani kurudisha pesa…