– Elijah Gicharu alisema uchunguzi wake katika mfuko wa CDF umeonesha Kuria amewapa kandarasi zenye thamani ya zaidi ya KSh 170 milioni jamaa zake
– Alisema Moses Kuria anapaswa kuondolewa afisini kutokana na matumizi mabaya ya mamlaka
– Alidokeza kuwa tayari amewasilisha stakabadhi za uchunguzi wake kwa EACC
Mkaazi wa Kiambu amewasilisha kesi ya kutaka mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria kuondolewa afisini kwa madai ya matumizi mabaya ya mamlaka katika utoaji wa kandarasi.
Elijah Kimani Gicharu alisema uchunguzi wake katika mfuko wa fedha za maendeleo ya maeneo bunge umeonesha Kuria amewapa kandarasi zenye thamani ya KSh 170, 878, 413 jamaa zake.
Kimani, katika malalamishi yake alidai kuwa ndugu wengine wawili wa mbunge huyo, John Nome Kuria na James Koigwho ambao ni wakurugenzi wa Supreme General Traders Ltd walipewa kandarasi ya jumla ya KSh 5,808,468 katika Shule ya Sekondari ya Mutungu.
Zaidi ya hayo, alisema Lujatech Enterprise Ltd, kampuni ambayo wakurugenzi wake ni Charles Regeru Nguru (kaka), Jane Muthoni Regeru (Dada-mkwe), Lucy Wambui Regeru (mpwa) na Teresia Mwihaki Regeru (mpwa) wa mbunge huyo wa Tanga Tanga walipewa zabuni yenye thamani ya KSh.10,267,955.
Mkazi huyo alisema pia dadake mwanasiasa huyo, Jane Wambui Kuria, alipokea kandarasi yenye thamani ya KSh 9,814,240 katika shule mbili kupitia kampuni yake ya Kiki Holdings Ltd.
John Ngige Kuria, mkurugenzi wa kampuni ya Numerical Strength Ltd pia inasemekana alipokea kandarasi ya KSh 31,525,120.