GAVANA wa Mombasa, Bw Hassan Joho, anaandamwa na kesi baada ya mke wake kuwasilisha ombi la talaka.
Mwanamke huyo anayetambuliwa kwa jina Madina Giovanni Fazzini, amedai kuwa gavana huyo amemtelekeza pamoja na watoto wake.
Katika hati zilizo mbele ya Mahakama ya Kadhi mjini Mombasa, mlalamishi anataka mahakama hiyo imsaidie kuvunja ndoa hiyo akidai amekuwa mpweke kwa zaidi ya miaka minane.
Aliyekuwa Naibu Gavana wa Mombasa Bi Hazel Katana (kushoto) akiwa na Mke wa Gavana Hassan Joho ambaye ni Bi Madina Joho na Bi Asli Sarai, ambaye ni mke wa aliyekuwa Seneta wa Mombasa Hassan Omar wasikiliza hotuba wakati wa Eid Baraza Julai 19, 2015. PICHA | MAKTABA
Kulingana naye, aliishi pamoja na Bw Joho tangu walipooana hadi mwaka wa 2013, ambapo anasema gavana huyo alihama nyumbani kwao.
“Tangu Bw Joho alipoondoka nyumbani, msingi wa ndoa yetu umeyeyuka na ndoa hii haiwezi kuendelea kudumu, iwe ni kwa msingi wa kisheria au kijamii,” akasema Bi Fazzini.
Rekodi za mahakama zinaonyesha kuwa wawili hao walioana kupitia kwa Sharia ya Kiislamu katika ndoa ya kukata na shoka ambayo ilifanywa Februari 11, 2011.
Tangu hapo, waliishi pamoja kama mume na mke hadi Januari 2013 ambapo waliachana, kisha Bw Joho akahama kutoka kwao mnamo Juni 2013.Mwanamke huyo ameambia mahakama kuwa, ameishi kwa upweke nyumbani kwao tangu alipotelekezwa.
“Ni wazi kuwa hakuna matumaini yoyote wala uwezekano wa kurudiana kwa njia yoyote ile kati yangu na mshtakiwa (Joho),” akasema.
Bi Fazzini alizidi kueleza kuwa, hajashirikiana kwa njia yoyote na mumewe kuwasilisha kesi hiyo mahakamani.
“Mlalamishi anawasilisha ombi kuwa agizo litolewe ili ndoa kati yake na mshtakiwa ivunjwe,” akasema, na kuongeza kuwa mahakama iko huru kutoa maagizo mengine yoyote ambayo yataonekana kufaa kwa kuzingatia jinsi kesi ilivyo.
Amelalamika kuwa gavana huyo alimwacha pamoja na watoto wake mnamo Juni 2013, miezi mitatu tu baada ya kushinda ugavana wa Kaunti ya Mombasa.
“Aliniacha na watoto Juni 2013. Tangu hapo nimekuwa nikiishi peke yangu,” akasema.
Bi Fazzini aliambatisha cheti cha ndoa yao na vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wao wawili walio na umri wa miaka tisa na minane, ambao anasema baba yao ni Bw Joho.
Madina Giovanni. PICHA | MAKTABA
Hakuwasilisha ombi jingine lolote kando na kutaka ndoa ivunjwe.
Alisema kando na kesi hiyo ambayo aliwasilisha Januari 26, hakuna kesi nyingine yoyote kati yake na Bw Joho kuhusiana na suala la talaka.
“Ninaapa katika hati hii kutetea ombi lililowasilishwa hapa, na ninafanya hivi nikitambua fika kwa ufahamu, habari na imani zangu isipokuwa kama kuna sehemu yoyote kuliko na maelezo tofauti,” akasema.
Mwanamke huyo ameagizwa kuwasilisha stakabadhi za kesi hiyo kwa Bw Joho.
Kufikia wakati wetu kuchapisha gazeti hili, Bw Joho hakuwa amewasilisha majibu kuhusu ombi hilo.Amepewa siku nne kuwasilisha majibu yake kwa Mahakama ya Kadhi kabla ya korti hiyo kutoa uamuzi.