Mlipuko wa trela la mafuta waua 77 Haiti
Na AFP
CAP-HAITIEN, Haiti
IDADI ya watu waliofariki kutokana na mkasa wa mlipuko wa trela la mafuta nchini Haiti jana Alhamisi ilifika 77 huku hofu ikitanda kwamba huenda idadi ya vifo ikaendelea kuongezeka.
Watu wengine 59 jana Alhamisi walikuwa wakitibiwa majeraha ya moto kufuatia mkasa huo uliotokea Jumatano asubuhi, mkurugezi wa idara ya kushughulikia masilahi ya raia Jerry Chandler aliambia AFP.
Kisa hicho kilitokea Jumatano jioni baada ya trela la kusafirisha mafuta kuanguka katika barabara moja yenye shughuli nyingi jijini Cap-Haitien.
“Wakati huu, tunaendelea na juhudi za kuimarisha uwezo wa hospitali kushughulikia waathiriwa wa mkasa huo,” akasema Chandler huku akiongeza kuwa hospitali moja iliyoko katika kituo cha mazoezi ya viungo iko tayari kuwahudumia waathiriwa.
Chandler alisema hospitali zinatarajiwa kuhudumia wahasiriwa kwa siku 10 zijazo, baada ya kupokea vifaa kutoka kwa Shirika la Afya Duniani (WHO) na wahudumu kutoka Wizara ya Afya nchini Haiti.
Watu wengi walijeruhiwa wakati wapita njia walifurika hapo kuchukua mafuta hayo- ambayo ni bidhaa adimu kutokana na uhaba wa mafuta unaokumba nchi hiyo wakati huu.
Baadhi ya wagonjwa walihamishwa hadi hospitali zilizoko nje ya jiji la Cap-Haitien, ikiwemo hospitali moja inayosimamiwa na Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) wenye wataalamu wa kutibu majeraha ya moto.
“Tumekuwa tukifanya kazi usiku kucha,” Mshirikishi wa Huduma za Afya wa MSF Jean Gilbert Ndong akasema.
“Wakati huu, wagonjwa 12 walioletwa hapa wanaendelea kupata nafuu,” akaeleza, akiongeza kuwa wanatarajia kupokea wagonjwa wengine baadaye.
Naibu Meya wa Cap-Haitien alitaja mkasa huo kama mbaya zaidi akisema “niliona watu wakiteketea wakiwa hai na haikuwa rahisi kuwatambua”.
Nyumba za makazi zilizoko karibu ziliharibiwa baada ya kushika moto kufuatia mlipuko huo.
Haiti haizalishi kiwango tosha cha stima kinachoweza kukimu mahitaji ya wakazi wake.
Hata katika maeneo kunakoishi matajiri katika jiji kuu, shirika la kusambaza stima nchini humo kutoa kawi hii kwa saa chache kwa siku.
Ukosefu wa mafuta pia umesababishwa na hatua ya magenge ya wahuni kuzingira hifadhi ya mafuta, hali ambayo imeathiri utoaji huduma za afya.
“Watu wengi wanaishi katika umasikini mkubwa,” akasema Marie-Rosy Auguste Ducena, mwanachama wa kundi kutetea haki la Nationali Network for the Defence of Human Rights.
“Umasikini ndio uliwasukuma watu kuenda kuchota mafuta kutoka kwa trela. Walidhani wangeuza mafuta hayo,” akasema.
Haiti ilitumbukia katika misukosuko mnamo Julai mwaka huu Rais Jovenel Moise alipouawa.
Waliopanga mauaji hayo hawajapatikana mpaka sasa.
Next article
WANDERI KAMAU: Mvutano wa Mahakama, Afisi ya Rais hatari…