MPC yaandaa matembezi ya kuhamasisha wanawake wajue haki zao
NA SAMMY KIMATU
WANAWAKE wameshauriwa kusimama kidete kuwania viti katika nyadhifa mbalimbali na wakome kasumba ya kuona wanaume pekee ndio walizaliwa viongozi.
Akiongea mnamo Jumamosi, Ofisa wa Masuala ya Rasilmali katika Mukuru Promotion Centre (MPC) Bi Lorraine Amondi Ogolla aliambia wasichana kujituma katika uongozi.
Bi Lorraine alisema hayo katika hafla ya kusherehekea Siku ya Wanawake Ulimwenguni iliyopangwa ba MPC na kushirikisha wakazi katika maeneo ya Mukuru, kaunti ya Nairobi.
“Nia ya hafla hii ni kuhamasisha jamii kuhusu nafasi ya mwanake kwa jamii na kuzitambua na kutumia fursa zilizopo katika ujenzi wa taifa. Hata hivyo, tuliandaa hafla yetu siku chache kwa kuchelewa baada ya hafla nyingine kusherehekewa kote nchini. Hii ilitokana na changamoto za wanafunzi ambao walikuwa wakifanya mtihani wa kitaifa huku sisi tukiwa na nia ya kuwa nao siku ya leo,” Bi Lorraine akaambia Taifa Leo.
Bi Lorraine alisema washiriki wengi walitoka mitaa ya mabanda ya Mukuru, lakini wengine walikuwa wageni kutoka mataifa kama vile Ireland, Marekani na Finland.
Baadhi ya wakazi wa Mukuru watembea wakitoa hamasisho kwa jamii ifahamu haki za mwanamke katika jamii. Matembezi hayo yaliandaliwa na Mukuru Promotion Centre (MPC), Machi 13, 2022. PICHA | SAMMY KIMATU
Aidha, aliongeza kwamba zaidi ya watu 200 walishiriki matembezi ili kuhamasisha jamii kuhusu kuzijua na kutekeleza haki za wanawake.
Washiriki walitembea kutoka Shule ya Msingi ya St Bakhita, barabara ya Likoni, barabara ya Entreprise, barabara ya Kayaba/ Hazina hadi barabara ya Aoko kuelekea shule ya Songa Mbele.
Katika shule ya Songa Mbele, washiriki walipumzika kwa muda huku wageni rasmi wakitoa hotuba zao wakiongozwa na mkurugenzi mkuu wa MPC, Mtawa Mary Killeen.
Mmoja wa wazungumzaji aliye kadhalika mhudumu wa jamii, Bw Joseph Otieno alisema mwanamke ni nguzo kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Kadhalika, alisema kuna umuhimu wa mwanamke kuwezeshwa ili jamii ifaidike kupitia kwake.