WAKAZI katika mtaa wa mabanda wa Kayaba, kaunti ndogo ya Starehe wamekosa maji kwa zaidi ya mwezi mmoja baada ya matapeli kudaiwa kuathiri mradi wa maji unaotegemewa na wakazi.
Aidha, mifereji imekauka tangu maji yakosekane kutoka kisima cha maji katika shule ya Msingi ya Sancta-Maria Mukuru.Mkuu wa shule hiyo, Bi Regina Nzomo aliambia wanahabari maji ya kisima shuleni ni mradi wa rais Uhuru Kenyatta chini ya idara ya Huduma ya Jiji la Nairobi (NMS).
Hata hivyo, Bi Nzomo alisema kwamba matapeli wanaouza maji mtaani wa mabanda wa Kayaba wamejiunganishia maji na kusabisha hitilafu katika mashine ya kupiga maji.
“Baada ya mtambo wa maji kuvurugwa na wakiritimba mtaani waliojiunganishia maji kuelekea mtaani, mashine ya kupiga maji imeharibika,” Bi Nzomo akateta.Usimamizi wa shule umeiomba serikali kutuma waandisi ili kukarabati mashine ndiposa shule na wakazi wapate maji.
Mradi huo wa maji ni wa tatu kuwekwa katika maeneo ya South B ikiwemo kisima cha St Bakhita na kile cha Hazina.Wakazi katika mitaa ya Hazina na Kayaba huchota maji kutoka kwa visima hivyo bila malipo yoyote.
PICHA/SAMMY KIMATU
Mkuu wa tarafa ya South B, Bw Michael Aswani Were alikashifu kitendo hicho na kutoa onyo kwa wanaohusika katika sakata ya maji.Vilevile, Bw Were aliongeza kwamba watakaopatikana na makosa ya ‘kuiba’ maji kupitia kujiunganishia paipu zao kwenye laini ya mradi huo watakamatwa na kufunguliwa mashtaka.
“Serikali ilichimba visima hivyo miongoni mwa vingine mitaani ya mabanda katika kaunti ya Nairobi ikilenga kuwapunguza wakiritimba ambao huwafyonza wananchi hela nyingi wanazotoza wakazi kutokana na huduma ya maji, stima na kodi ya nyumba,” Bw Were asema.
Kwa sasa, wakazi walikosa maji ya mgao kutoka siku ya Alhamisi hadi tukienda mitaboni.Maji ya mgao husabazwa na Kampuni ya Maji na Maji Taka (NCW&SC).Wachuuzi huuza maji kwa Sh5 kwa kila mtungi wa lita 20 lakini wakati kuna uhaba wa bidhaa hiyo, hupandisha na kuuza Sh10 na Sh20 kwa kila mtungi mmoja wa maji wa lita 20.
Vilevile, mwenyekiti wa usalama mtaani wa mabanda wa Kayaba, Bw Jacob Ibrahim alisema wakati kuna uhaba mkubwa wa maji mtaani, NMS hupeleka maji na malori ili kuwasabazia wakazi bila kuwatoza ada yoyote.
Wakati mwingine, serikali kupitia NMS huwasabazia maji wanayopeleka kwa malori mitaani bila kulipisha pesa.“Wakati hali imekuwa mbaya zaidi na wakazi wetu hawapati maji ya kampuni ya NSW&SC, huwa tunawasiliana na viongozi wetu kisha tunaletewa maji na malori ya NMS bila malipo yoyote,” Bw Jacob Ibrahim akanena.