Connect with us

General News

Msako mkali dhidi ya disko matanga kuanza – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Msako mkali dhidi ya disko matanga kuanza – Taifa Leo

Msako mkali dhidi ya disko matanga kuanza

NA KNA

SERIKALI imeamua kuanzisha msako mkali dhidi ya watu wanaoendeleza hafla za ‘disko matanga’.

Kamishna wa eneo la Pwani, Bw John Elungata, alisema hafla hizo za usiku huchangia kwa aina mbalimbali za uhalifu akasisitiza kwamba serikali imejitolea kuzikomesha.

Wiki iliyopita, Taifa Leo ilibainisha bado kuna changamoto kuzima hafla hizo ambazo serikali ilikuwa imepiga marufuku, hasa katika kaunti za Kwale na Kilifi.

“Polisi wataendeleza msako kukamata wale wanaoendeleza biashara hii ya utamaduni uliopitwa na wakati,” akasema, akiwa afisini mwake Mombasa.

Disko matanga wakati mwingi huandaliwa usiku katika matanga au mazishini, na huvutia watoto wa umri mdogo ambapo imebainika baadhi ya washichana huishia kutungwa mimba.

Wakati uo huo, Bw Elungata aliwashauri wazazi kulinda watoto wao wakati wanapokuwa katika likizo ya muda mrefu.

Bw Elungata alisema ni muhimu wazazi wahakikishe kuwa watoto wao hawajitosi kwa maovu na aina nyingine za uhalifu.

“Ni muhimu wazazi kuhakikisha watoto wao wako salama na wafuatilie shughuli zao kwa karibu wakati huu wa likizo,” akasema.

Alisema wageni wanaopanga kutembelea kaunti za Pwani wahakikishe watakuwa wakiandamana na watoto wao wakitaka kuogelea, ili kuepusha visa vya watoto kufa maji.

Kando na hayo, Bw Elungata alisema maandalizi ya Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE) eneo hilo yamekamilika. Mtihani huo umeanza leo Jumatatu.

Aliagiza maafisa wa usalama waliopewa jukumu la kutoa ulinzi katika vituo vya mitihani wahakikishe watahiniwa wote na vifaa vya mitihani vitakuwa salama katika kipindi kizima cha mitihani hiyo.