Msamaha kwa wanasiasa wamletea DPP shida tele
Na RICHARD MUNGUTI
HATUA ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji ya kuchelea kuwafungulia mashtaka wanasiasa wafisadi kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022 imezua cheche za kisheria huku Rais Uhuru Kenyatta akiombwa amtimue kazini.
Katika kesi iliyowasilishwa na mwanaharakati Charles Rubia katika mahakama kuu , uamuzi huo wa Haji wadaiwa kuwabagua wananchi wa kawaida wanaosukumwa kortini kila mara kwa makosa wanayoshtakiwa. “Uamuzi wa Haji wa Aprili 11, 2022 unakinzana na katiba inayosema kila mmoja yuko sawa na mwingine na wakosaji waadhibiwe barabara,” asema Rubia katika kesi iliyoshtakiwa na mawakili Danstan Omari na Martina Swiga.
Katika uamuzi huo Haji alisema “hatawashtaki magavana , wabunge na wanasiasa wanaohusika na ufisadi katika kipindi hiki cha kampeini.” Hatua hii , mahakama kuu imeelezwa ni ubaguzi mtupu kwani wananchi wanaendelea kufikishwa kortini kwa mashtaka mbali mbali kila uchao.
Katika kesi hiyo Rubia anaomba mahakama kuu iharamishe uamuzi huo wa Haji kwamba hatawashtaki wanasiasa wanaopora mabilioni na matrilioni ya pesa za umma kabla uchaguzi mkuu kufanyika. Rubia anasema , Haji amekaidi katiba na kipengele nambari 157 cha katiba kinachompa uwezo na mamlaka ya kumfungulia kesi kila anayevunja sheria.
“Kwa mujibu wa kifungu nambari 143 cha katiba ni Rais tu asiye weza funguliwa mashtaka akali afisini,”asema Rubia. Mwanaharakati huyu amedai uamuzi huo wa Haji umepotoka na unakinzana na katiba. Mlalamishi huyu anaomba mahakama kuu isitishe uamuzi huo na kuamuru Haji ajiuzulu huku mkurugenzi wa jinai (DCI) na inspekta jenerali wakichunguza uhusiano kati ya kiongozi huyu wa mashtaka na wanasiasa.
Rubia aliyewashtaki DPP , na asasi kadhaa za serikali ikiwamo ile kamati inayosimamia utekelezaji wa haki (NCAJ) ambayo kinara wake ni Jaji Mkuu Martha Koome anaomba korti imchukulie hatua kali. “Ni bunge tu inayoweza kubadili sheria na kutoa matamshi kama hayo ya kusamehe wafisadi na wala sio Haji,”asema Rubia. Mahakama imeelezwa tume ya kupambana na ufisadi (Eacc) ilikamilisha uchunguzi wa zaidi ya kesi 5,000 lakini Haji amekataa kuidhinisha mashtaka yawasilishwe kortini.
Pia mahakama imeelezwa kuna magavana watatu ambao Haji hajawafungulia kesi licha ya mapendekezo kutolewa na Eacc. Mahakama imeelezwa kuwa uamuzi huo wa Haji wa kutowashtaki wanasiasa “ni mfano mbaya machoni pa umma.” Korti imeambiwa uamuzi huu unazorotesha juhudi zilizowekwa kupambana na uozo wa ufisadi unaopepeta sekta ya umma.
Mahakama imeelezwa Haji amejitwika jukumu la kuwaidhinisha wanaoshtakiwa ilhali kuna maafisa 2,500 waliohitimu. “Uamuzi huu wa Haji unapinga utekelezwaji wa ajenda kuu nne za Rais Uhuru Kenyatta anayechangamkia uangamizaji wa ufisadi, ”alisema Bw Omari alipowasilisha kesi hiyo.
Next article
Klopp aingia nusu fainali UEFA