[ad_1]
Mshukiwa mmoja akamatwa, polisi wapata lita 38 za pombe haramu Makongeni
Na SAMMY KIMATU
MSHUKIWA mmoja amekamatwa na maafisa wa polisi waliofanikiwa kutwaa lita 38 za pombe haramu ya chang’aa wakati wa msako dhidi ya vileo vilivyoharamishwa na serikali.
Operesheni hiyo ilifanyika katika mtaa wa Makongeni kwenye kaunti ndogo ya Makadara.
Kamanda wa polisi katika eneo la Makadara, Bw Timon Odingo aliambia Taifa Leo msako huo ulifanikishwa na juhudi za wakazi kupasha polisi habari.
Zaidi ya hayo, Bw Odingo aliongeza kwamba mshukiwa aliyekamatwa alikuwa ni mwanamke.
Japo misako ya polisi hufanywa mara kwa mara, Bw Odingo alisema siku hizi, washukiwa wamebuni mbinu mpya ya kuuza pombe haramu mitaani.
“Sababu wanajua polisi ni lazima wafanye misako, hao hutoa pombe kidogo ya kuuzia wateja wao huku wakificha pombe ile nyingi katika stoo mbali na wanakouza pombe ili polisi wakiwakamata, wapate pombe ndogo,” Bw Odingo akasema.
Kwa upande mwingine, aliwapongeza raia kwa kupasha polisi habari, jambo lililochangia washukiwa kunaswa na pombe nyingi kuharibiwa.
“Baada ya kufanya msururu wa misako mitaani, kwa kweli uuzaji wa pombe haramu ya chang’aa imepungua kwa kiwango kikubwa,” Bw Odingo akaongeza.
Wakati huo, kamanda Odingo aliwashauri wanaume kuzingatia ndoa zao akiongeza kwamba unywaji wa pombe ya chang’aa na pombe zingine haramu umechangia pakubwa ndoa nyingi kusambaratika.
“Nawaomba wanaume kujihusisha na masuala yanayoweza kuwasaidia maishani na kuinua uchumi wa taifa nikisema wanawake wengi wanahusisha kuvunjika kwa ndoa zao na hunywaji wa pombe haramu ya chang’aa,” Bw Odingo akanena.
[ad_2]
Source link