Msururu wa ahadi hewa za Naibu Rais
NA PETER MBURU
KAMPENI za Ikulu za Naibu Rais William Ruto zimetawaliwa na ahadi nne kuu za kiuchumi ambazo ni sawa na alizowapa Wakenya pamoja na Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2017, lakini wakakosa kuzitimiza.
Badala yake, Dkt Ruto sasa anarusha lawama kwingineko anapojaribu kuelezea sababu za ahadi hizo kufeli.
Wakati huu, anamimina ahadi hizo akijua wazi bado masuala muhimu yaliyothibitishwa na watafiti kwamba, ndiyo kizingiti kwa utekelezaji wa ahadi hizo.
Hivyo, kwa kujivumisha kupitia ahadi hizo hizo, ni kujikweza kisiasa akitumia hila.
Dkt Ruto amekuwa akisisitiza kuwa, pamoja na wandani wake wa kisiasa, wamekubaliana kuzingatia masuala manne muhimu, ikiwa ni pamoja na kuwekeza Sh100 bilioni kwa miradi na mipango itakayowapa vijana nafasi milioni nne za ajira.
Amekuwa akiahidi kuwa atafanikisha hili kwa kuwa serikali itaongeza kiwango cha pesa katika sekta za ujenzi wa nyumba za bei nafuu na viwanda pamoja na kilimo ili nafasi zaidi za ajira zipatikane.
Lakini mwanya mkubwa katika ahadi hii ni kuwa, tayari bajeti ya mwaka anaorejelea imeshapangwa na serikali kuhusu mipango itakayofadhiliwa 2022/23 na hivyo haelezi atakapotoa pesa hizo za ziada.
Pia, Dkt Ruto hajafafanua kipya atakachofanya kuhakikisha kuna mazingira bora ya kuinua sekta hizo zizalishe ajira. Hazungumzii jinsi atasuluhisha changamoto ambazo wafanyabiashara hupitia, zikiwemo kutozwa ushuru wa juu, bei ya juu ya nguvu za umeme, nyenzo za kufanyia kazi, na mazingira mengine yanayozibana.
Kulingana na ripoti kuhusu ushindani wa viwanda duniani, sekta ya viwanda Kenya inaorodheshwa 115 kati ya 152, hivyo Kenya ni mojawapo ya nchi duniani zenye mazingira mabaya kwa ustawi wa viwanda. 5.8%
Asilimia ya Wakenya waliosajiliwa kunufaika na mpango wa Afya kwa Wote unaofadhiliwa na serikali ya Kenya.
Bila kushughulikia haya na kufafanua jinsi atayashughulikia, Dkt Ruto bado haonyeshi atafanya chochote tofauti na kile serikali imekuwa ikifanya kumaliza njaa inayoathiri takriban Wakenya milioni tatu kwa sasa.
Ahadi nyingine kuu ambayo Naibu Rais amerejelea katika kampeni zake ni kwamba, kufikia mwishoni mwa mwaka huu, kila Mken – ya atapata bima ya kitaifa ya afya (NHIF.
“Kabla ya Desemba, kila Mkenya atakuwa na bima ya NHIF, na yule ambaye hana pesa za kulipia, serikali ya Kenya itamlipia ili kila mmoja wetu aende hospitalini, atibiwe na aende nyumbani bila kulipishwa chochote,” akasema.
Mbali na kutofafanua atakapotoa pesa hizo ikizingatiwa kuwa tayari bajeti ya mwaka anaorejelea imepangwa, Dkt Ruto hazingatii kuwa utafiti umebaini kuna mseto wa changa – moto zilizozuia serikali ya Jubilee kuwalinda Wakenya wote kiafya kupitia mpango wa UHC.
“Kufikia 2021, ni Wakenya milioni tatu pekee waliokuwa wamesajiliwa kunufaika na mpango wa UHC. Hii ni asilimia 5.8 ya Wakenya. Mapengo yaliyopo katika nguzo hii ni kutokana na utekelezaji mbaya wa mipango muhimu kama kufadhili hospitali kwa vifaa spesheli (MES), Mpango wa Linda Mama, uajiri wa wafanyakazi wa afya na upanuzi wa vituo vya afya,” Kamati ya Bunge kuhusu Afya ikasema katika ripoti.