JARIDA la GQ liliripoti kuwa katika enzi za maisha yake, Castro alishiriki mapenzi na wanawake takriban 35,000.
Kati ya hao, alioa wawili tu. Jamaa alivuta pumzi yake ya mwisho Novemba 2016 akiwa na miaka 90.
Kati ya viwembe hawa sijui ni yupi Diamond Platnumz anafukuzia rekodi yake. Ukiachana na ustaa na ustaha wake, Mondi kathibitisha vilevile kuwa ni ‘fisi’ mmoja hatari kama walivyokuwa Castro na Mfalme Suleimani.
Kiumbe chochote kile chenye sauti nyororo, mapaja manene, kashepu ka’ chupa ya CocaCola hivi kitakachomvutia, hakimpiti kwa urahisi.
Jamaa kavuruga takriban mataifa yote ya Afrika Mashariki na wakati mwingi kila anakotua, anaacha mbegu. Taarifa mpya zinaarifu kuwa kwa sasa yupo kwenye mahusiano na msanii wake Zuchu. Hebu tujikumbushe kidogo kuhusu jamaa na Ma-Ex wake.
ZUHURA ‘ZUCHU’ OTHMAN
Mamake Khadija Kopa alipompeleka bintiye pale Wasafi-WCB, hakutegemea kabisa ingefikia hapa.
Alichotaka ni kumsaidia bintiye kutimiza ndoto yake ya kuwa staa mwanamuziki. Hiyo ndoto aliifanikisha kupitia sapoti ya Diamond.
Sasa taarifa zilizotolewa na mpambe wake Juma Lokole ni kuwa Diamond kaamua kwenda hatua zaidi na kuanza kummega mtoto wa watu.
Mwanamuziki Zuchu. PICHA | HISANI
Kopa awali alikana ila sasa amerithia mahusiano hayo. Tayari kuna tetesi za ndoa. Ila hili sio jipya kulisikia kutoka kwa Mondi. Tusichokijua ni ikiwa Zuchu naye ni wingu la kupita au ndio Mondi kakusudia kweli kutulia.
TANASHA DONNA
Mrembo huyu ndiye aliyeiwakilisha Kenya kwenye listi ndefu ya mademu wa jamaa. Baada ya mahusiano ya usiri wa miezi minane hivi, waliweka penzi lao hadharani Oktoba 2019. Mwaka mmoja baadaye penzi likaingia mdudu na wakaachana. Tanasha alidai walitofautiana kimawazo na kimtazamo.
Taarifa za Bongo ziliarifu kuwa Diamond hakupendelea kabisa Tanasha afanye muziki lakini binti wa watu akawa king’ang’anizi. Hapo jamaa akajikata. Lakini wakati wanaachana, tayari alikuwa ameshamwaga mbegu na akamzalia Naseeb Junior.
ZARI HASSAN
Anashikilia rekodi ya kuwa miongoni mwa wanawake wachache waliofanikiwa kudeti jamaa kwa miaka kadhaa. Uhusiano wao ulidumu kwa takriban miaka minne katika kipindi ambacho walijaliwa watoto wawili.
Kukawa na stori za ndoa. Zari akasubiri kuposwa nusura Yesu amkute. Kutokana na umbali kati yao ikizingatiwa Zari anaishi Afrika Kusini, Mondi akaanza kuhanya. Zari akajua. Akamsamehe mara ya kwanza, ila alipohanyiwa mara ya pili, mrembo huyo akaamua kumbwaga siku ya Valentino 2018.
HAMISA MOBETTO
Ukipenda unaweza ukamwita anavyoitwa na Watanzania wenzake ‘Miss Magodoro’. Watanzania wanamini kuwa lile shepu la Hamisa hasa mwonekano wa makalio yake huwa sio asili. Wamedai kuwa Hamisa huvalia mavazi speshio ya magodoro ili yamfanye aonekane vile kiasi cha kumpagawisha hata rapa Rick Ross.
Hamisa Mobetto. PICHA | MAKTABA
Lakini kabla Ross amjue, mrembo huyu anayependa kuvuruga mastaa ndiye aliyepasua uhusiano wa Zari na Mondi. Wakati Zari akiwa Sauzi, Hamisa alitumia fursa hiyo kupasha joto kitanda chao. Akanasa mimba na Mondi alipojaribu kuikana, akamwanika. Ndio sababu Zari alimtema.
Mnakumbuka Mondi akisema yupo radhi kutambaa kwa magoti hadi Sauzi akamwombe msamaha Zari? Chanzo, ile mimba. Baada ya kuachwa na Zari, alilipiza kisasi kwa kumtema Hamisa kwa kumwanika wakati muda wote walikuwa wakikanyagana chini ya maji.
WEMA SEPETU
Miss Tanzania 2006 ndiye anashikilia rekodi ya kudeti Mondi kwa muda mrefu zaidi. Kwa zaidi ya miaka mitano, walideti wakiachana.
Wema alimkuta Mondi akiwa mshamba. Ndio mwanzo jamaa alikuwa anaanza muziki.
Mwanamitindo Wema Sepetu. PICHA | MAKTABA
Wema ndiye alimfunza jamaa Kizungu ila mpaka leo bado hunoa tu. Ilitajwa kuwa kapo bora Afrika Mashariki. Mwisho wa siku Mondi alimchoka na kumtema na ndipo alipotua kwa Zari.
JOKATE ‘KIDOTI’ MWEGELO
Kwa sasa ndiye mkuu wa Wilaya ya Dar es Salaam. Jokate alikuwa mshikaji wa miaka mingi wa Wema. Wote walikuwa ni mamodo. Kwenye shindano la Miss Tanzania 2006, Jokate alimaliza wa pili. Walikuwa ni ma-bestie hata baada ya shindano. Lakini waliishia kujengeana bifu baada ya Mondi kuanzisha uhusiano wa kimya kimya na Jokate huku akiwa na Wema.
Kwa wanawake wote aliotoka nao, Mondi amewahi kukiri kuwa anajutia kumuumiza Jokate kwa sababu alimaucha bila ya sababu yoyote. Alimtaja kuwa mwanamke bomba. Uhusiano wa Jokate, Mondi na Wema hadi wa leo kidogo hauna ukaribu.
PENNIEL ‘PENNY’ MUNGILWA
Alikuwa ni mwigizaji na mtangazaji. Lakini pia alikuwa ni shogake Jokate na Wema. Naye alijikuta kwenye utandu wa Mondi na waliishia kuyaweka mahusiano yao wazi 2013 baada ya jamaa kumtema Wema. Mondi alimwacha kwa madai ya kuwa alitoa mimba yake. Hebu nenda ukasikize mashairi ya kibao Sikomi.
JACKLINE WOLPER
Huyu ni mmoja wa wanawake wakongwe kwenye showbiz ya Tanzania. Alipata umaarufu kipindi sanaa ya filamu Tanzania ilikuwa ikilipa sana. Aliwahi kuwa side-chic wa Mondi kipindi jamaa akiwa anatoka na Wema. Baadaye aliingia kwenye uhusiano na Harmonize alipokuwa chini ya lebo ya Wasafi.
TUNDA SEBASTIAN
Pengine ndio uhusiano wa kimya kuwahi kuwa kati ya Diamond na mwanamke. Tunda alinaswa kwenye utandu wa Mondi baada ya jamaa kuachwa na Zari 2018. Hata hivyo yaliyokuwa yakiendelea baina yao yalikuwa ni kufurahishana tu kwa kutoana uchu. Hawakufika mbali.
IRENE UWOYA
Mwigizaji huyu wa Bongo Movie naye alinaswa kwenye utandu huo. Wandani wanasema kuliwahi kuwepo na kitu kati yao licha ya wawili hao kuishi kusisitiza ni marafiki. Baada ya kumalizana, Uwoya akaanza kuonekana na Lava Lava.