Connect with us

General News

Mung’aro aanza kumponda Kingi – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Mung’aro aanza kumponda Kingi – Taifa Leo

Mung’aro aanza kumponda Kingi

NA ALEX KALAMA

ALIYEKUWA Waziri Msaidizi wa Ugatuzi, Bw Gideon Mung’aro, amemtaka Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi, kukoma kutumia hafla rasmi za serikali ya kaunti kuendeleza siasa za uchaguzi ujao.

Wiki iliyopita, Bw Kingi alifanya ziara katika maeneo mbalimbali ya Kilifi ambapo alitembelea miradi ya maendeleo lakini hotuba zake zikashamiri masuala kuhusu chama chake cha Pamoja African Alliance (PAA), na mipango ya chama hicho kuelekea kwa uchaguzi ujao na baadaye.

Bw Mung’aro ambaye amepanga kushindania tikiti ya ODM kuwania ugavana kaunti hiyo alisema mienendo hiyo ni makosa akidai kuwa inaashiria fedha za umma zinatumiwa kuandaa mikutano ya kuuza sera za chama hicho.

Kando na hayo, alitilia shaka pia ahadi ambazo gavana huyo amekuwa akidai zitafanikishwa kupitia kwa PAA akisema Bw Kingi alikuwa na muda wa vipindi viwili vya ugavana kutoa uongozi ambao ungeletea wananchi yale anayowaahidi sasa.

“Habari za kuanza kudanganya watu eti ukileta chama kitatatua matatizo haya, utafanya kupitia sheria ipi? Masuala ya kuanza tena kuzungusha watu kuwaambia eti chama ndio kitasaidia, chama kitafanya kazi chama ni dau la kukupeleka wewe hatua nyingine?” akasema Bw Mung’aro.

Wakati Bw Kingi alipokutana na wanachama wa PAA Kilifi wiki iliyopita, alilaumu marais waliotangulia kwa kushindwa kutatua changamoto za umiliki wa ardhi, kulinda rasilimali muhimu za eneo hilo na viwanda vikubwa, hali ambayo iliporomosha uchumi wa Pwani.

Kulingana naye, masuala hayo yanaweza kuangaziwa vyema ikiwa Pwani itapata sauti huru katika meza ya uongozi wa kitaifa, kupitia kwa chama kilicho na mizizi yake ukanda huo ndiposa akajiunga na PAA.

“Lazima tupange mikakati ili kuhakikisha kuwa ahadi za viongozi zinazotolewa wakati wa kampeni wanapotafuta kura zetu zitatekelezwa kikamilifu baada ya uchaguzi. Bila hilo, jamii ya Wapwani itaendelea kukosa sauti,” alisema Bw Kingi.

Chama hicho ambacho kinatarajiwa kujiunga na Azimio la Umoja kupitia kwa mkataba na Jubilee, kinaunga mkono Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga kwa uchaguzi wa urais.

Hata hivyo, wanasiasa wa ODM katika Kaunti ya Kilifi hupingana na PAA wakisema kinataka kutumia umaarufu wa Bw Odinga kuzoa viti vingine vya kisiasa katika kaunti, maeneobunge na wadi.

Bw Mung’aro alisisitiza kuwa, ikiwa Bw Kingi ni mwaminifu, aeleze wananchi utawala wake ulifanikisha kubuniwa kwa nafasi ngapi za ajira alipokuwa mamlakani.

“Atuambie alikuwa ameandika watu wangapi wa Kilifi,” akasema Bw Mung’aro.

Aliyekuwa spika wa bunge la kaunti ya Kilifi, Bw Jimmy Kahindi, alidai kuwa uongozi wa kaunti haukutilia maanani miswada muhimu iliyopitishwa na bunge la kaunti hiyo ambayo ingesaidia wananchi.

“Sisi kama bunge tumekuwa tukipitisha bajeti pale bungeni. Ni kwa sababu gani miaka kumi ya ugatuzi hatuna maji ndani ya Kilifi?” alisema Bw Kahindi.

Diwani wa Malindi Mjini, Bw David Kadenge ambaye ni mfuasi wa PAA aliwataka viongozi hao kukoma kushambulia gavana Kingi na badala yake watafute njia za kujieleza kwa wanainchi.

“Ikiwa kweli wanaona wana ushahidi wa kuonyesha Gavana Kingi anatumia fedha za wananchi ili kuuza sera za PAA basi waende wakaandikishe taarifa kwa polisi badala ya kueneza porojo zisizokuwa na mshiko,” akasema.

Alizidi kusema, Bw Kingi hatafuti kiti chochote bali ni wao ambao wanatafuta viti na hivyo basi wanafaa kutumia muda wao kuambia wananchi yale ambayo watawafanyia.

“Hicho ndicho kitu muhimu wanataka kusikia lakini sio kueneza habari za uongo. Ukiona watu kama hao jua ni viongozi ambao wamekosa ajenda za kuwaambia wanainchi sasa wameona njia pekee ambayo wanaweza kutumia kujipigia debe ni kumtukana Gavana Kingi,” akasema.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Facebook

Trending