NJENJE: Majanichai: Munya awaagiza wadau kulainisha mifumo ya uuzaji
NA WANDERI KAMAU
WAZIRI wa Kilimo, Peter Munya, amewaagiza wadau katika sekta ya kilimo kufanya utafiti kubaini sababu ya bei za majanichai kushuka kwenye Soko la Uuzaji Majanichai la Mombasa.
Wakulima wamekuwa wakilalamika kwamba mapato yao bado yako chini, licha ya serikali kuweka mikakati kuyaboresha.
Bw Munya alitoa makataa ya wiki mbili kwa Bodi ya Majanichai Kenya (TBK), kumteua mhasibu kukagua kwa kina mfumo unaotumiwa na Chama cha Majanichai Afrika Mashariki (EATTA), ili kubaini utaratibu wa kuamua bei za vipimo tofauti vya zao hilo.
Kwa muda mrefu, serikali imekuwa ikiwalaumu wasimamizi wakuu wa soko hilo kwa kushirikiana na mawakala kuamua bei za zao hilo, hali ambayo huwanyima wakulima mapato kutokana na mauzo yake.
“Kuna haja kuchunguza utaratibu na mfumo unaotumika kuamua bei za zao hilo ili kuhakikisha hautumiwi na yeyote kuvuruga vipimo vya majanichai kuwalaghai wakulima kwenye malipo yao. Kumekuwa na malalamishi mengi sana kutoka kwa wakulima kuhusu kiwango cha majanichai wanayouza na malipo wanayopokea,” akasema Bw Munya.
Kama njia ya kuhakikisha uwazi kwenye taratibu za kuamua bei za zao hilo, Wizara ya Kilimo iliwaagiza wasimamizi wa soko hilo kuanza kutumia mfumo wa kielektroniki na kuacha ule wa kawaida.Afisa Mkuu Mtendaji wa TBK, Bi Perris Mudida, alisema kuwa tayari wameanza harakati za kumtafuta mhasibu kuendesha mchakato huo.
“Kwa sasa tunabuni utaratibu ambao utatumika kama mwongozo kuendesha mageuzi hayo. Ni mchakato unaoendelea,” akasema Bi Mudida.
Bw Munya alisema mageuzi hayo yanalenga kuwaepushia wakulima ulaghai ambao umekuwa ukiendeshwa dhidi yao na mawakala wasiowajali.Kulingana na mapendekezo hayo, mifumo yote ya mauzo ya majanichai inapaswa kugeuzwa kuwa ya kidijitali katika viwanda vyote kote nchini.
“Kwa miezi mitatu ijayo, tutaanza kutekeleza mapendekezo hayo kwa kina ili kuhakikisha tumerejesha imani ya wakulima kwenye sekta hii,” akasema.
Next article
Ajichumia hela mjini katika ufugaji mbalimbali